USTAWI wa afya ya akili ya mama wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua ni suala muhimu, lakini utafiti umebaini halipewi kipaumbele nchini.
Imebainika kuwa, kutokana na suala hilo kutopewa kipaumbele, kinamama wengi wanakosa msaada, hivyo kupata madhara yanayotajwa kuchangia ongezeko la wagonjwa wa akili nchini.
Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Kliniki Kilimanjaro mwaka 2018 kwa wanawake 1,128 wilayani Moshi, ulibaini kwamba, mmoja kati ya 10 (asilimia 12.2) alikuwa na changamoto ya afya ya akili ya baada ya kujifungua.
Utafiti mwingine uliofanywa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) mwaka 2015 kwa wajawazito 1,180, ulibaini kwamba, wanane kati ya 10 (asilimia 78.2) walikuwa na shinikizo la damu na dalili za wasiwasi wakati wa ujauzito.
Hospitali hiyo ya ngazi ya juu zaidi kitaifa, pia ilibaini kuwa asilimia 49 ya kinamama hao 1,180 waliokuwa na ujauzito, walikuwa na dalili za mfadhaiko.
Maria Gregory (40), mkazi wa Mbezi, wilayani Ubungo, mkoani Dar es Salaam, anasimulia alivyochoshwa na vilio visivyokoma vya mtoto wake mchanga, hata kufikiria kujiua.
"Mtoto alikuwa analia usiku kucha, mume wangu akahama chumbani na kuniachia mzigo wa kubembeleza mtoto huku ninauguza kidonda, maana nilijifungua kwa upasuaji.
"Kutokana na uchovu niliokuwa ninapata kutokana na misukosuko ya malezi na kelele hizo za mtoto, nikapata hisia za kumchukia mwanangu. Usiku nilikuwa ninachoka na kuhisi kuchanganyikiwa.
"Mtoto anataka umbebe tu, ukimlaza analia, sikuwa na msaada na nilijikuta mtoto anapolia, ninalia naye na kuna wakati nilipata mawazo ya kujiua.
"Hata nilipomshirikisha mama yangu mzazi kuhusu madhila haya, alinishauri niende kanisani kuombewa kwa kuwa aliona ajabu 'mama kuchukia mtoto wake mchanga', akahisi nimepatwa na mapepo," Maria anasimulia.
Mama huyo wa watoto watatu mwenye shahada ya ualimu, anasema kuwa na msongo huo wa mawazo kwa miezi mitatu, alipokwenda kliniki, alimweleza muuguzi kuhusu hali yake; naye akashauri apumzike kwa muda mrefu, jambo ambalo lisingewezekana kwa kuwa hakuwa na mtu wa kumsaidia kazi za nyumbani.
"Nilipata hofu kwamba ningekufa na kuacha watoto wangu wakiteseka. Nikaperuzi mtandaoni kuhusu ile hali na namna ya kukabiliana nayo. Nilipanga ratiba ya kupumzika wakati wa mchana mama alipokuja kunisalimia.
"Baadaye nikaajiri yaya wa kusaidiana naye kulea mtoto usiku, na nikatafuta msaada wa kiroho kutoka kwa wachungaji, miezi sita baadaye nilipona kabisa," Maria anasema.
Tatu Athumani ni mama wa watoto watatu kama ilivyo kwa Maria, tofauti yao yeye ni mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam na ni mdogo kwa miaka miwili kwa maana ana umri wa miaka 38.
Anasema kuwa, baada ya kujifungua mtoto wake wa tatu (wa kike), alijikuta akielemewa na kazi za nyumbani huku akiwa na mtoto mwingine mdogo mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.
"Sikutaka kuhudumiwa na mtu yeyote. Hapo nilikuwa na watoto wengine wawili; mkubwa alikuwa na umri wa miaka minne na alihitaji kuandaliwa kila siku kwa ajili ya kwenda chekechekea (shule ya awali).
"Nilijikuta nina uchovu sana na hasira mara kwa mara. Wakati mwingine nilijifungia chumbani na kulia kutokana na kuhisi upweke hadi mume wangu aliporejea nyumbani jioni na kunisaidia baadhi ya kazi.
"Msaada wa mume wangu haukuwa mkubwa kwa sababu alikuwa anashinda kazini muda mwingi, alikuwa anarejea nyumbani saa 10 jioni na kuondoka alfajiri.
"Nilidumu katika hali hiyo kwa takribani miezi minane nisijue la kufanya, marafiki zangu wakanishauri kuvumilia kwa maelezo kuwa hata wao walipitia hali hiyo na ikaisha. Baadaye nilipata akili ya kuleta msaidizi, nikapata nafuu," Tatu anasema.
Farhat Rashid, mkazi wa Unguja, anasema alipata msongo wa mawazo wakati baada ya mumewe kumwacha na kuoa mke mwingine wakati akiwa na ujauzito wa miezi sita.
"Nilipopata taarifa ameoa, nikawa na mawazo na maswali mengi yasiyo na majibu, muda mwingi nilijifungia chumbani peke yangu na kulia, hadi pale mama alipomweleza daktari wakati wa kliniki, akanitafutia mtaalamu wa saikolojia, akanisaidia kukubaliana na hali ya kuachwa, nikapata nafuu," anasema Farhat.
Daktari wa Magonjwa ya Wanawake MNH, Benny Kimaro anasema anakutana na kesi tatu hadi nne kila mwezi za wanawake wanaopata changamoto ya afya ya akili baada ya kujifungua.
Dk. Kimaro anasema ugonjwa huo huathiri kinamama baada ya kujifungua na dalili hutokea kati ya siku ya tatu hadi tano baada ya kujifungua.
"Mama anapitia hisia hasi kama vile upweke, kulia mara kwa mara, kutopenda mtoto wake. Kama akichelewa kupata matibabu, anaweza kumdhuru hata mwanae.
"Ni hali inayosababishwa na mambo mbalimbali, ikiwamo mabadiliko ya homoni wakati wa ujauzito, ujauzito usiotarajiwa, changamoto za kiafya kama vile shinikizo la damu na ukosefu wa msaada wakati wa miezi ya mapema ya utunzaji mtoto," Dk. Kimaro anasema.
Kukabaliana na maradhi hayo, Dk. Kimaro anashauri wanaume washiriki kikamilifu kulea watoto katika miezi ya mwazo ya mtoto na kutowanyanyapaa wenza wao pale wanaoonesha dalili za afya ya akili, bali wawapeleke kituo cha afya.
Msaikolojia Tiba kutoka Kituo cha Afya Somedics, jijini Dar es Salaam, Dk. Saldin Kimangale anasema wanawake wanaopata tatizo hilo, hukosa furaha, usingizi, hamu ya kula, na kuwa mtazamo hasi kuhusu wao wenyewe, hasira na msongo wa mawazo.
Dk. Kimangale anashauri wanawake kujiepusha na mimba zisizotarajiwa na elimu itolewe katika kliniki za wajawazito ili watambue na kujiepusha na visababishi vya ugonjwa huo pamoja na kuhakikisha wanapata msaada wa kutosha baada ya kujifungua.
"Mgonjwa wa afya ya akili anapopeletwa katika kituo chetu cha afya huwa tunamtibu kulingana na ukubwa wa tatizo; kuna wanaohitaji ushauri nasaha, wengine vidonge na wale walioathirika zaidi hulazwa katika vituo maalum, ikiwamo kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Milembe," anasema.
Dk. Luzango Maembe, Mtaalamu wa Magonjwa ya Wanawake katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa Mwananyamala, Dar es Salaam, anathibitisha hospitali hiyo kupokea wagonjwa wanawake wenye changamoto za afya ya akili, wengi wakifikishwa hospitalini huko ugonjwa ukiwa umefika katika hatua ya mwisho ya kuhitaji kulazwa.
Anashauri jamii ipewe elimu ya mara kwa mara ili ione ugonjwa huo kama magonjwa mengine na mgonjwa apelekwe kituo cha afya pale tu anapoonesha dalili za mwanzo badala ya kusubiri mpaka aathirike zaidi.
Kwa Tanzania, mtumishi mwanamke akijifungua anapewa siku 84 za likizo ya uzazi kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini huku mumewe akipewa siku tatu za kusaidia malezi ya mtoto aliyezaliwa.
Shabani Mwinyiheri, mkazi wa Temeke, Dar es Salaam, anashauri sheria hiyo ifanyiwe maboresho ili kumwongezea baba muda wa kukaa nyumbani kumsaidia mama kulea angalau kwa mwezi mmoja.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, akiwasilisha bungeni Mei mwaka huu makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2024/25, alisema kwamba, hadi kufikia Julai 2023, kulikuwa na wagonjwa 293,952 waliohudhuria katika vituo vya kutolea huduma za maradhi ya afya ya akili Tanzania Bara.
Pasi na kutaja idadi halisi ya kinamama waliokumbwa na maradhi ya afya ya akili baada ya kujifungua, Waziri Ummy alisema wagonjwa afya ya akili 19,506 waliripotiwa kulazwa hospitalini mwaka 2023/24 kulinganisha na wagonjwa 13,262 waliolazwa mwaka wa 2022/23.
Alisema takwimu hizo zinaonesha kuwapo kwa ongezeko la uelewa wa jamii kuhusu suala hilo na kuwapo vituo vya afya vinavyotoa matibabu kwa kundi hilo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED