RC Kunenge atoa maagizo mazito kwa wakuu wa Wilaya Pwani

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 05:49 PM Sep 05 2024
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge
Picha: Julieth Mkireri
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge amesema wakuu wa wilaya zote za mkoa huo wanatakiwa kufanya kulingana na uwezo wao sambamba na kufanya maamuzi sahihi ambayo yatachochea ukuaji wa maendeleo katika wilaya zao.

Kunenge  ametoa maagizo hayo Mjini Kibaha wakati wa hafla fupi ya kumuapisha Mkuu mpya wa Wilaya ya Rufiji, Luteni Kanali Fredrick Komba ambaye ameteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan  kushika nafasi hiyo hivi karibuni.

Mkuu huyo wa mkoa amewataka viongozi hao  kufanya kazi kwa uadilifu na kuondoa urasimu ambao unaweza kukwamisha juhudi zinazoendelea kufanywa na Serikali ya uchumi kwenye uwekezaji wa viwanda.

Kunenge pia ametoa maelekezo kwa wakuu wa wilaya za mkoa huo kusimamia utekelezaji wa ilani sambamba na kushirikiana na CCM katika utendaji wake wa kazi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Luteni Kanali Fredrick Komba ameahidi kufanya kazi kulingana na kiapo chake  ili kuhakikisha maono  ya Serikali kuhusiana na maendeleo yanafikiwa.