Rais Samia afuta sherehe za Uhuru

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:40 AM Dec 05 2024
Rais Samia Suluhu Hassan.
Picha: Mtandao
Rais Samia Suluhu Hassan.

RAIS Samia Suluhu Hassan amefuta maadhimisho ya dherehe za miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwa mwaka 2024 na kuelekeza yafanyike katika ngazi ya mikoa.

Licha ya kufuta maadhimisho hayo, Rais Samia ameelekeza fedha zilizotengwa katika kila taasisi kwa ajili hiyo, zielekezwe katika kutoa huduma za kijamii.

Pia ameelekeza kila mkoa uhakikishe wilaya zake zinafanya shughuli za kijamii ikiwamo upandaji miti, usafi wa mazingira katika maeneo ya kijamii kama vile  masoko, hospitali, kambi za wazee na wenye mahitaji maalum.

Kadhalika, ameagiza kufanya mashindano ya michezo mbalimbali pamoja na makongamano na midahalo ya kujadili maendeleo endelevu ambayo nchi imefikia katika kipindi cha miaka 63 ya Uhuru. 

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema hayo jana jijini Dodoma katika kikao kazi cha mawaziri kilichofanyika katika ukumbi wa Hazina.

“Sherehe za mwaka huu hazitakuwa na gwaride na shughuli zingine za kitaifa,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa. 

 Badala yake, alisema serikali inatoa wito kwa wananchi kushiriki katika shughuli hizo ili kujivunia sifa za kipekee ambazo zimetokana na Uhuru.

“Ninatoa rai kwa wakuu wote wa mikoa kuzingatia na kufuata ipasavyo maelekezo mahsusi yaliyotolewa na serikali ili kuhakikisha maadhimisho haya yanafanyika kwa ufanisi kwa lengo la kuuenzi Uhuru wetu,” alisema.

Majaliwa alisema shughuli za maadhimisho zilishaanza tangu mwanzoni mwa mwezi huu na zitafanyika hadi siku ya kilele ambacho ni Desemba 9, mwaka huu.

“Katika maadhimisho haya, taasisi zote za serikali na vyombo vyote vya ulinzi na usalama zinaelekezwa kuhakikisha majengo yote ya serikali Tanzania Bara yanapambwa kwa vitambaa vya rangi ya bendera ya Taifa.

“Picha rasmi ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye ni Muasisi wa Uhuru wetu pamoja na picha ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ziwekwe,” alisema.

Maadhimisho hayo yanabebwa na kauli mbiu isemayo “Miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara: “UONGOZI MADHUBUTI NA USHIRIKISHWAJI WA WANANCHI NI MSINGI WA MAENDELEO YETU.”