Prof. Janabi: Matibabu ya Kibingwa yagharimu bil 1.439/-

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 05:58 PM Jul 20 2024
Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Prof. Mohamed Janabi.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Prof. Mohamed Janabi.

SERIKALI imegharamia matibabu ya kibingwa kwa wagonjwa 24 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kwa ajili ya upandikizaji wa figo na uloto pia vifaa vya usikivu, kwa gharama ya Sh. bilioni 1.439.

Huduma hizo za upandikizaji na vifaa vya usikivu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano, zimefanyika kwa kipindi cha mwaka 2023/2024.

Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Prof. Mohamed Janabi, alisema hayo akitoa taarifa ya utekelezaji wa program ya utoaji huduma bingwa na bobezi, kwa madaktari wazawa kutoka MNH, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH).

Prof. Janabi alisema kwamba MNH ilipokea Sh. billioni 2.6 kwa ajili ya kuwatibu wagonjwa waliofika hospitalini hapo, ili kupata huduma za kibingwa, akisema kwa siku wagonjwa wanaosafishwa figo kwa siku MNH hufikia 100 hadi 150.

“Program hii imefadhiliwa na Rais. Dk. Samia imesaidia kuokoa maisha ya wenzetu, kwa sababu gharama za kutibu figo ni Sh. milioni 30. Kupandikiza uloto Sh. milioni 69 na kifaa vya usikivu ni Sh. milioni 45,” alisema Prof. Janabi.

Alitaja baadhi ya sababu zinazochangia ugonjwa wa figo, ni unywaji holela wa dawa za kupunguza maumivu, shikizo la juu ya damu, kisukari na magonjwa mengine, kama vile malaria.

Kuhusu tatizo la usikivu kwa watoto Prof. Janabi, amewaasa wazazi na walezi kutowaadhibu watoto pindi wanapohisi hawawasikilizi badala yake wafike katika vituo vya kutolea huduma kubaini tatizo, ili kuanza tiba kabla ya kufikisha umri wa miaka mitano.

Bingwa wa Magonjwa ya Figo, Dk. Jonathan Mngumi alisema serikali imefanya uwekezaji mkubwa wa vifaa na wataalam kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa kwa asilimia 70.

“Wagonjwa wanaopata matibabu wanaendelea na maisha, kwa sababu mtu anaweza kuishi na figo moja bila tatizo lolote jambo la msingi ni kuzingatia mtindo bora wa maisha.
 
Bingwa wa Masikio, Pua na Koo (ENT), Dk. Aslam Nkya, alisema hadi sasa wameshafanya oparesheni kwa wagonjwa 87 na tangu, Rais Samia aingie madarakani huku wagonjwa 31 wakitibiwa na madaktari bingwa wazawa.

“Tumebaini changamoto kwa watoto wanaofika kutokana na tatizo la usikivu, wengi wao wanafika umri ukiwa zaidi ya miaka mitano, wakati kitaalam tunashauri wawe na umri angalau miaka miwili,” alisema Dk. Nkya.

Katika kuhakikisha  wanawafikia watoto wenye tatizo la usikivu, hospitali imeanzisha kampeni ya kuwapima watoto wote wanaozaliwa MNH, kubaini iwapo wana tatizo na wakibainika wapate matibabu mapema.

Utafiti unaonyesha kuwa kati ya kinamama 1,000 wanaojifungua, watoto wanne wanazaliwa na tatizo la usikivu.

Balele Edward, aliyekuwa anasumbuliwa na figo, alisema alipandikiziwa figo ilyotoka kwa mama yake, baada ya kugundulika na tatizo hilo mwaka 2018. 

Asha Athumani, ambaye mama yake alitoa figo kwa ajili yake, kwa sasa amepona na anaendelea vizuri na kufanikiwa kupata watoto wawili.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, alisema katika mwaka wa fedha 2023/2024, serikali ilitoa Sh. bilioni 5.6 kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa na bobezi kutoka kwa MNH wakipata Sh. bilioni 2.6, BMH Sh. bilioni moja na JKCI Sh. milioni 900.

Alipongeza huduma zinazotolewa na MNH, kuahidi kuongeza bajeti, ili wagonjwa wengi wanufaike na kwamba mwaka 2024/2025 Sh. bilioni sita zimetengwa, kwa ajili ya kutoa huduma za matibabu katika hospitali hizo.

“Moyo wangu unafarijika kuona namna madaktari wetu wazawa wanavyotoa huduma za kibingwa hapa nchini, wananchi walikuwa wanatumia gharama kubwa kwenda nje ya nchi lakini sasa zinapatikana hapa. Vipaumbele vya wizara ni kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa gharama nafuu kuimarisha huduma,” alisema  Ummy.