Nyongo: Wananchi Maswa wanasafiri kwenda Bariadi kuhifadhi maiti

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 10:41 PM Apr 16 2024
Mbunge wa Maswa Mashariki (CCM), Stanslaus Nyongo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mbunge wa Maswa Mashariki (CCM), Stanslaus Nyongo.

Mbunge wa Maswa Mashariki (CCM), Stanslaus Nyongo amesema wananchi wa Wilaya ya Maswa kwa takriban wiki tatu hawana jokofu la kuhifadhi maiti na kulazimika kusafiri umbali wa kilomita 50 kwenda kuhifadhi Wilaya ya Bariadi.

Akiuliza swali la nyongeza bungeni leo, Nyongo amesema lini wananchi watarejeshewa huduma hiyo na jokofu lililoharibika uwezo wake ulikuwa ni kuhifadhi miili mitatu na kuhoji serikali kama itakuwa tayari kupeleka lenye Uwezo mkubwa.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dk.Festo Dugange akijibu swali hilo, ameagiza uongozi wa Hospitali ya Maswa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kuhakikisha jokofu lenye uwezo mkubwa linapatikana ndani ya wiki moja.

"Hospitali ya Wilaya ya Maswa inapaswa kuwa na jokofu linalofanya kazi naomba Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kufanya tathmini ya jokofu linalotakiwa kwa ajili ya kutunza miili katika hospitali hiyo na ndani ya wiki moja liwe limepelekwa ili huduma ziende vizuri,"amesema.