Mbwa 12 waua watoto wawili wa familia moja

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:22 PM Dec 08 2024
Mbwa
Picha: Mtandao
Mbwa

WATOTO wawili wa familia moja wamefariki dunia, baada ya kushambuliwa, kujeruhiwa tumboni na mbavuni na mbwa 12, wakati wakielekea shule ya msingi Izia, iliyoko manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa leo na Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, tukio hilo limetokea Desemba 6, mwaka huu, majira ya saa 3:00 asubuhi wakati watoto hao ni Faidha Daudi (13) na Issa Siku (11) ambao ni mtu na mdogo wake, wakielekea shuleni.

Amesema tukio hilo lilitokea katika mtaa na kata ya Katandala na kwamba kundi la mbwa zaidi ya 12 wanaomilikiwa na mtu au watu tofauti ambao hawajajulikana liliwavamia na kuwashambulia watoto hao, kiasi cha kusababisha majeraha katika miili yao hasa maeneo ya tumboni na mbavuni.

“Polisi kwa kushirikiana na Ofisa Mifugo wa Manispaa ya Sumbawanga, baada ya tukio hilo waliwaangamiza mbwa watano wanaozagaa mtaani, ikiwa ni mwendelezo wa operesheni maalum ya kuondoa mbwa hao mtaani,” amesema.

Aidha, amesema polisi wanaendelea na uchunguzi, ili kuwabaini wamiliki wa mbwa hao kwa ajili ya kuchukua hatua za kisheria.

“Polisi tunatoa wito kwa wananchi wanaomiliki wanyama wakali kama mbwa kuwadhibiti kwa kuwafungia, ili kuepusha madhara kwa binadamu. Pia tunawataka wazazi na walezi kuwakanya watoto wao kuhusu tabia za kuwachokoza mbwa mtaani,” amesema.