MBUNGE wa Jimbo la Ngorongoro, Emmanuel Ole Shangai, amesema madiwani,kamati ya siasa na viongozi wa kimila Leigwanani,katika kikao cha ndani na Katibu wa NEC,Itikadi,Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla,wamefikisha kero zote za wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro ambazo wanataka zifike kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza leo Septemba 6,2024 kwenye mkutano wa hadhara mjini Karatu,mkoani Arusha,amesema katika kikao hicho wamefikisha sauti za wananchi kwa kuwa kiongozi huyo ameshindwa kwenda eneo hilo kutokana na katazo la polisi.
Agosti 24,mwaka huu,polisi walikataa ombi la CCM kwenda eneo la Ngorongoro kutokana na katazo la lililotolewa na Jeshi la Polisi Wilaya ya Ngorongoro.
Mbunge huyo alimshukuru Makalla kwa kikao cha ndani cha madiwani,Leigwanani na kamati ya siasa Wilaya ya Ngorongoro na kwamba wamemweleza changamoto zao ambazo wanaamini atazifikisha kwa Mwenyekiti wa CCM taifa, Rais Samia.
"Wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro tupo naye (Rais Samia), tunaamini zilizopo zitatuliwa,tumezileta kwako ili zifike,"amesema.
Aidha, amesema eneo la Ngorongoro limepata miradi mingi ya maendeleo ikiwamo shule tano za sekondari hospitali ya wilaya,barabara yenye urefu wa kilomita 49 na zahanati.
Mbunge huyo amesema kuna changamoto kadhaa ikiwamo ubovu wa barabara ya Kigongo hadi Sale wilayani humo na kwamba ni wilaya pekee ambayo haijaunganishwa na Mkoa na kwamba wakitaka kwenda Ngorongoro ni lazima wafunge mikanda kwasababu ya barabara mbovu.
"Tukitaka kupeleka bidhaa au wananchi wa Karatu wakitaka kuleta kule (Ngorongoro) wanakosa kutokana na barabara mbovu,tunaomba serikali itujengee hii barabara,"amesema mbunge huyo.
Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Dadi Kolimba, amesema wilaya hiyo imepokea Sh.bilioni 27.6 ambazo nyingi zimekwenda kwenye elimu na shule mpya saba huku shule kongwe ya Karatu iliyopewa mil 700 na kwamba matokeo ya kidato cha nne hakuna daraja la nne na sifuri jambo ambalo linaonyesha ni hatua kubwa.
Amesema walipokea bil 2.2 kwa ajili ya ukarabati wa Hospitali ya Wilaya ambayo inahudumia wagonjwa 500 hadi 800 na kwamba huduma ya mama na mtoto inatolewa bila tatizo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED