Mbowe ataka serikali 'ifunge mkanda'

By Restuta James , Nipashe
Published at 11:14 PM Jun 27 2024
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),  Freeman Mbowe.
Picha: Mtandao
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe.

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, ametahadharisha kuhusu matumizi ya fedha za umma, akiitaka serikali ibane matumizi.

Mbowe ametoa tahadhari hiyo kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii leo Juni 27, 2024; akionya kwamba nchi haiwezi kuendelea ikiwa asilimia 89 ya pato la nchi itatumika kulipa madeni na kuendesha serikali.

"Kama nchi, tunalipa wakati huo huo tunaendelea kukopa  mikopo mikubwa. Serikali ya CCM haioni umuhimu wa  kupunguza matumizi ili kuelekeza sehemu kubwa zaidi ya  bajeti kuletea Watanzania maendeleo; tuwapumzishe," amesema.

"Katika pato la taifa kwa mwaka tunatafuna asilimia 89 kwa mambo mawili; madeni (asilimia 51) na  matumizi ya serikali (asilimia 38). Pesa kidogo  iliyobaki haikidhi kuendesha miradi ya  maendeleo katika nchi hii."