Matumbo joto uteuzi CHADEMA

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 01:49 PM May 16 2024
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mrema.
Picha: Maktaba
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mrema.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema majina ya watiania katika nafasi mbalimbali za uongozi kwenye Kanda yanatarajiwa kutangazwa wakati wowote huku kikiwataka watakaokatwa kukubali matokeo.

Mchujo wa watiania hao ulimalizika usiku wa kumkia jana.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mrema, amesema watiania watakaokatwa inabidi wakubali matokeo kwa kuwa zipo kazi nyingine za chama watakazoendelea kufanya.

“Tukikamilisha uteuzi tutawajulisha ambao wameteuliwa na ambao hawakuteuliwa. Maana ya usaili ni kwamba tuna vigezo vyetu kwa mujibu wa katiba na kanuni yetu, ni sifa gani viongozi wa ngazi gani wanapaswa kuwa nayo,” amesema Mrema.

“Kama mtu akikutwa hana hizo sifa, basi moja kwa moja anaweza akaenguliwa, atashauriwa atumikie majukumu mengine kwa sababu bado ni chama kimoja, nafasi ni chache, wanachama wote hawawezi kuwa viongozi.”

Mmoja wa maofisa wa chama hicho ameliambia gazeti hili kuwa majina ya wasailiwa yanatarajiwa kutolewa wakati wowote ndani ya siku mbili kuanzia jana.

“Jana (juzi), Kamati Kuu ilimaliza kazi ya kuchuja majina ya wasailiwa wote na sasa kinachosubiriwa ni kutoa majina ya watakaoteuliwa ambayo wakati wowote yatatolewa, kama sio kupitia mkutano na waandishi wa habari, lakini itatolewa taarifa kwa umma,” amesema.

Kwa mujibu wa Mrema, kanuni ya 7.5 ya chama hicho, yenye vipengele zaidi ya 13 inaeleza sifa ambazo kila mgombea kulingana na nafasi yake anatakiwa kuwa nazo.

“Nafasi ya Mwenyekiti inaeleza anatakiwa awe na sifa gani, Katibu, Mwenezi na nyinginezo ziko kwenye kanuni za chama,” amesema Mrema.

Amesema watiania waliosailiwa katika kanda hizo nne ni 136, wanao tiania kwenye nafasi za mabaraza na za chama.

Awali, kikao hicho kilipangwa kifanyike siku tatu, lakini kilifanyika kwa siku nne.

“Awali, kikao chetu kilipangwa kifanyike kwa siku tatu, lakini Kamati Kuu ililazimika kukisogeza mbele kwa siku moja. Katika kikao hiki tumekuwa na ajenda nyingi mojawapo ikiwa kupokea taarifa ya uchaguzi wa ngazi za mikoa, wilaya, majimbo, kata, mitaa, vijiji na misingi kwa nchi nzima pamoja na kufanya uteuzi kwa wagombea wa kanda nne za Victoria, Serengeti, Magharibi na Nyasa,” amesema Mrema.

Mada nyingine zilizojadiliwa katika kikao hicho cha Kamati Kuu ni pamoja na kupokea taarifa ya chaguzi, kupokea tathmini ya maandamano ya awamu ya kwanza ya mikoa na kuweka mwelekeo wa awamu ya pili ya maandamano na kufanya usaili wa kuteua wagombea nafasi za uongozi katika kanda nne.

Katika siku zote hizo nne za kikao cha Kamati Kuu, yapo mambo mengi yaliyokuwa yanajitokeza hususani kwa watiania waliokuwa wameweka kambi makao makuu ya chama hicho Mikocheni kwa siku mbili kusubiri kusailiwa ikiwamo majigambo.

Miongoni mwa majigambo yalikuwa ya kutunishiana ‘misuli’ ya nani anaweza kukatwa na nani anaweza kubaki wakihusisha historia zao katika eneo la nidhamu ndani na nje ya chama, misimamo yao na namna ya kushinda mitego mbalimbali inayohusu hujuma za chama chao hasa kuelekea kipindi cha uchaguzi.

Kadhalika, wapo baadhi walisikika wakiwa na mazungumzo ya kutamani wasikie kauli ya chama kuhusu kile kinachodaiwa kuwapo fedha chafu ndani ya chama hicho hasa katika maeneo yanayofanya uchaguzi.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara Mei 2, mwaka huu, Makamu Mwenyekiti Bara wa chama hicho, Tundu Lissu, alitamka hadharani kwamba ndani ya chama hicho kuna harufu ya fedha chafu ambazo zimemwagwa kuvuruga uchaguzi.