Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, amepiga marufuku hospitali kuzuia maiti kwa mwananchi kutokana na gharama za matibabu na badala yake zibuni njia mbadala za kudai malipo hayo.
Makonda ametoa agizo hilo leo alipofanya ziara katika hospitali ya Wilaya ya Monduli kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la mionzi na la upasuaji.
Amesema wajitahidi kuwa na huruma na kuwapunguzia wananchi maumivu wanapoona hali zao ni mbaya kifedha badala ya kuendelea kuzuia maiti.
Aidha, amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa na Waganga wakuu wa wilaya zote za Mkoa wa Arusha kusimamia agizo hilo ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, alilolitoa kupitia kwa Waziri wa afya.
Makonda amewataka wahudumu wa afya mkoani Arusha kutoa huduma nzuri kwa wananchi wanaofika hospitalini na kwenye vituo vyote vya afya ili kuwa sehemu ya kuwapunguzia maumivu wananchi kutokana na magonjwa yanayowasumbua.
Amesema Mkoa wa Arusha unafaa kuwa mfano wa huduma nzuri za afya ili kuendana na uwekezaji mkubwa wa serikali ya awamu ya sita kutokana na Rais Samia kutoa fedha nyingi za kuwezesha miundombinu bora ya utoaji wa huduma za kiafya.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED