Mkuu wa Mkoa wa Arusha,Paul Makonda, amemtimua Ofisa Ardhi wa Halmashauri ya Arusha, Shevednaz Mwakyokola, katika mkutano wake na kuagiza polisi kumchukua kwa kuwa alimshuhudia akipokea rushwa ya Sh. milioni tano.
Makonda alifikia uamuzi jana jioni wakati akizungumza na wananchi wa Ngaramtoni Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha baada ya kufanya ukaguzi wa miradi.
"Hapa tulipo nimemuona mtumishi ambaye nilishasema sitaki kumuona ninataka achunguzwe lakini nimemuona yupo hapa Ofisa Ardhi njoo hapa … alikuwa amekaa hapo njoo upo chini ya ulinzi uchunguzi uendelee,” amesema Makonda na kuongeza kuwa;
“Nimemkuta kwa macho yangu anachukua Sh milioni tano ya rushwa simama wewe unajua njoo hapa TAKUKURU anzeni naye kwa macho yangu nimemuona alivyo mtu wa ajabu akaitupa ile hela ili asionekane na ushahidi upo nimeshasema ni bora siku moja nikae kinywani kwa bwana kuliko siku 1,000 nikae na wazalimu,”.
Makonda alisema siku aliyokuja Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi mkoani Arusha alimuona kwa macho yake anapewa fedha alimfuata na kumuambia ampatie hiyo bahasha akaitupa isionekane na ushahidi wa clip anao.
“Hatuwezi kuwa na watu wala rushwa wanakaa kwenye ofisi wanakandamiza haki za watu alafu tuwachekee sio mimi hilo sio la kwangua naomba tuelewane siwezi kuwabembeleza watumishi wazembe na wala rushwa”amesema Makonda.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED