Makamu wa Pili ataka wananchi kutembelea maonyesho

By Restuta James , Nipashe
Published at 06:32 AM Apr 20 2024
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla akiwaaga wananchi mara baada ya kufungua Maonesho ya Biashara Miaka 60 ya Muungano katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam jana.
Picha: Mpigapicha Wetu
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla akiwaaga wananchi mara baada ya kufungua Maonesho ya Biashara Miaka 60 ya Muungano katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam jana.

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, ametoa rai kwa wananchi kutembelea maonyesho ya taasisi za Muungano yanayoangazia miaka 60 tangu Zanzibar na Tanganyika zilipoungana, ili kufahamu huduma na kutoa maoni ya namna ya kuuimarisha.

Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akizindua maonyesho ya miaka 60 ya Muungano katika viwanja vya Mnazi Mmoja, yanayoshirikisha taasisi za muungano pamoja na wafanyabiashara wadogo.

Alisema katika maonyesho hayo, wananchi watapata fursa ya kufahamu huduma zinazotolewa na Taasisi za Muungano, mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 60 na watapata nafasi ya kutoa maoni na ushauri utakaowezesha kuimarisha na kuudumisha.

“Muungano Wetu unatimiza miaka 60 ambapo tumeshuhudia mafanikio makubwa katika maeneo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa kwa wananchi wa pande zote mbili za Muungano, wameendelea kunufaika kwa kuwapa fursa za kuishi kwa amani na kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo popote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania…umekuwa nyenzo na utambulisho muhimu wa umoja wetu,” alisema.

Alisema katika miaka 60 iliyopita, serikali za pande zote zimesimamia utekelezaji wa masuala ya Muungano kwa ufanisi mkubwa ambao umefanikisha kuimarisha kwa utaifa, umoja, amani, utulivu na hali ya maisha ya wananchi kutokana na ukuaji wa uchumi.

“Kuwapo kwa Muungano kumesaidia sana kuimarisha hali za wananchi na kuinua uchumi wa pande zote mbili za Muungano. Hali hiyo imetokana na kuwepo kwa soko la pamoja lisilokuwa na vikwazo vya kiutawala na kiuendeshaji linalojumuisha ushirikiano na utengamano unaorahisisha mtiririko wa rasilimali na bidhaa, mitaji, watu na huduma baina ya Tanzania Bara na Zanzibar,” alisema Makamu huyo wa Pili, Abdulla.

Alisema Muungano umeibua fursa nyingi za kibiashara katika sekta za viwanda, hoteli na kujenga nyumba za biashara na makazi ambazo zimeongeza ajira kwa wananchi wa pande zote mbili za Muungano.

Akizungumzia huduma za kijamii, alisema zimeimarika hususani za afya, maji, elimu, ustawi na maendeleo ya jamii na makazi na kwamba udugu wa damu umeimarika kwa kuwa wananchi wa pande zote za Muungano wameungana katika misingi ya ndoa na urafiki.

“Taasisi 33 zimefungua Ofisi Zanzibar kati ya Taasisi 39 za Muungano. Hii ni hatua kubwa katika kuimarisha huduma kwa wananchi wetu na kuimarisha Muungano. Natoa wito kwa zile ambazo bado hazijafungua Ofisi Zanzibar kufanya hivyo,” alisema.

Alisema ni wajibu wa kila Mtanzania kuulinda, kuuimarisha na kuudumisha akigusia kaulimbiu ya ‘Tumeimarika na Tumeshikamana kwa Maendeleo ya Taifa Letu.’

Awali, Naibu Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis, alisema maonyesho hayo ni mfululizo wa shughuli mbalimbali zinazoratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais katika kutoa elimu ya Muungano kwa makundi mbalimbali wakiwemo wananchi, wabunge, viongozi wa Serikali na wanafunzi.

“Tunapoadhimisha miaka 60 ya Muungano wetu, Watanzania wote tuna kila sababu ya kutafakari na kutathmini masuala muhimu yaliyokusudiwa na Waasisi wa Taifa letu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, ambao walitia saini Hati ya Makubaliano ya Muungano kwa niaba ya wananchi wa nchi hizi mbili,” alisema.

Alisema waasisi hao waliweka misingi ya haki kwa ajili ya kuimarisha umoja, amani na utulivu nchini.

Aidha, wakati wa maonyesho, wananchi watapata fursa ya kufahamu chimbuko, msingi na maendeleo ya Muungano.

“Kuanzia mwaka 2006 hadi 2024, hoja 25 zilipokelewa na kujadiliwa ambapo kati ya hoja hizo, 22 zimepatiwa ufumbuzi na kuondolewa kwenye orodha ya hoja za Muungano. Aidha, hoja zilizobaki zipo katika hatua mbalimbali za kupatiwa ufumbuzi,” alisema.

Ufunguzi wa maonyesho hayo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, watumishi, taasisi za serikali na wafanyabiashara.

Maonyesho hayo yanafanyika jijini Dar es Salaam na Zanzibar eneo la Nyamanzi, Fumba.