Makami wakomaa Kilema iwe barabara ya utalii

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 01:50 PM Jul 10 2024
Mkandarasi aliyepewa zabuni ya ujenzi wa barabara 11 za vijiji viwili vya Kata ya Kilema Kaskazini, akitia saini kandarasi ya kuanza kazi hiyo.
Picha: Godfrey Mushi
Mkandarasi aliyepewa zabuni ya ujenzi wa barabara 11 za vijiji viwili vya Kata ya Kilema Kaskazini, akitia saini kandarasi ya kuanza kazi hiyo.

VIJIJI viwili vya Makami Juu na Makami Chini vilivyoko Kata ya Kilema Kaskazini, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, vimeitaka Wizara ya Maliasili na Utalii na Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro (KINAPA), kuifungua barabara ya Kilema, ili kuanza kutumika kwa ajili ya shughuli za utalii.

Wameiomba serikali kutoitumia pekee kama barabara ya dharura, badala yake itumike kama barabara maalum ya kupandisha watalii kwenda Mlima Kilimanjaro.

Kwa nyakati tofauti jana wananchi wa vijiji hivyo, akiwamo Wolter Nguma, ambaye ni mdau wa maendeleo katika kata hiyo, ameiomba serikali kuifungua barabara hiyo ya Kilema, ili itumike kwa shughuli za utalii.

“Ndio maana tunazidi kupigania barabara hii ya Kilema iweze kufunguliwa kwa ajili ya shughuli za utalii. Isitumike tu kama barabara ya dharura, bali itumike kama barabara maalum ya kupandisha watalii kwenda Mlima Kilimanjaro.

“Maana yake ni kwamba kama barabara ya TANAPA ikijengwa vizuri, matokeo yake ni kwamba hivi vjijiji vingine hivi vitakuwa na uwezo sasa wa kuanza kujengwa hoteli na vitu vingine vya namna hiyo.

…Ukiangalia bado tunahitaji teknolojia kwenye masuala ya kilimo, migomba ambayo tunayoitumia sasa hivi bado ni ya kizamani, ukiangalia miti ya kahawa iliyoko bado ni ya zamani, kwa hiyo bado tunahitaji wale wataalamu wa kilimo kuja katika maeneo haya na kuweza kuleta mabadiliko.

Zaidi aliongeza: “Tumeanza sisi kama kikundi lakini tunaamini sasa kama serikali ikishirikiana na sisi, basi uwezekano wa kuwaondoa watu wetu wa maeneo haya katika umasikini ambao upo.”

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Makami Juu, Happynes Samweli, amewaunga mkono wananchi hao, akisema kama serikali itaridhia barabara hiyo kufunguliwa kwa ajili ya shughuli za utalii, itapunguza tatizo la umasikini wa kipato walichonacho wakazi wa kijiji hicho.

Kata ya Kilema Kaskazini, pamoja na mambo mengine haina Kituo cha Afya, wala Kituo cha Polisi.