Madaktari kicheko kikokotoo mafao

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:40 AM Jun 15 2024
Daktari.
Picha: Mtandao
Daktari.

CHAMA cha Madaktari Tanzania (MAT), kimetoa neno kuhusu kikokotoo cha wastaafu baada ya serikali kutangaza kuongeza mafao ya mkupuo kwa wastaafu na kueleza kuwa matamanio yao yalikuwa ni ongezeko kwa asilimia 50.

Juzi, serikali ilitangaza kwamba, watumishi ambao ni wanachama wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) sasa watapata mafao ya mkupuo kwa kikokotoo cha asilimia 40 badala ya asilimia 33 iliyoibua malalamiko.

Wenzao wa sekta binafsi walioko Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) nao wanatarajia kushuhudia ongezeko la mafao ya mkupuo, wakiwa na kikokotoo kipya cha asilimia 35 badala ya asilimia 33 iliyopo kisheria hivi sasa.

Katika maoni yao, siku moja baada ya Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, kuwasilisha bungeni mapendekezo ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2024/25,  Rais wa MAT, Dk. Deus Ndilanha, alisema wanashukuru kufikia asilimia 40, ingawa walitamani kingefikia asilimia 50.

 Dk. Ndilanha alisema wanatamani ingekuwa kwa asilimia 50 kwa kuwa umri wa madaktari bingwa kustaafu umeongezwa ikilinganishwa na watumishi wengine wa umma.

“Kwanza ifahamike kwamba madaktari ni sehemu ya watumishi wa umma na walioko sekta binafsi bahati mbaya na wao waliingia kwenye hiyo kadhia ya kushuka kwa kiwango cha mafao baada ya kustaafu.

“Kwa kweli walikuwa wanatamani sana kikokotoo kingebaki kama ilivyokuwa zamani asilimia 50 kwa fedha ya mkupuo, lakini kwa asilimia 40 tunashukuru, hoja yao kubwa ya madaktari umri wa kustaafu umeongezwa daktari bingwa umri wa kustaafu kwa lazima ni miaka 65 na kwa hiari ni 60.

“Tofauti na watumishi wengine wao kwa hiari ni miaka 55 kwa lazima ni umri wa miaka 60, utaona ni miaka mitano imeongezwa kwa madaktari, sasa alikuwa akistaafu kikokotoo chake ni asilimia 33 kilikuwa kinawaumiza zaidi kulinganisha na watumishi wengine,” alisema.

Dk.Ndilanha alisema asilimia 40 si mbaya lakini matamanio ya madaktari ingekuwa ni asilimia 50 ingekuwa nzuri zaidi.

“Hata hii asilimia 40 tunashukuru kwani inahakikisha hawa watu wanapata chao baada ya kutumikia serikali na umma muda wote mpaka wanastaafu,” alisema.

MAONI YA BAJETI

Kampuni ya kimataifa ya huduma za ukaguzi wa kitaalamu ya Ernst & Young (EY) imeonya kuhusu utegemezi wa fedha za wafadhili kutoka nje kuendesha miradi ya kimkakati ya maendeleo.

Meneja Mwandamizi wa Kodi kutoka EY, Fred Lugangira, alisema bajeti hiyo ni jumuishi kwa kuwa serikali imeweka malengo ya kimkakati na ubunifu ili kupanua wigo wa kodi na kuwezesha ulipaji wa kodi kwa hiari.

“Bajeti iliyowasilishwa inategemea mapato ya nje, ingawa suala hili haliepukiki, bado linahitaji kuchukuliwa kwa tahadhari kwa kubuni vyanzo vingi vya mapato kama ambavyo waziri amefanya.

“Waziri tayari amependekeza kuwa mamlaka za serikali za mitaa kubuni vyanzo vingi vya mapato ili kupunguza utegemezi wa mapato kutoka nje, huu ni mpango mzuri tunaposonga mbele,” alisema.

Aidha, alisema wameona namna kampuni za kimataifa zinavyosajiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)  ili kulipa kodi, lakini pia mikakati iliyowekwa na serikali ya kupata mikopo yenye masharti nafuu ili kufadhili miradi ya maendeleo.

Pia alisema ajali za barabarani ni miongoni mwa maeneo ambayo serikali imekuwa ikipoteza nguvu kazi na kwamba, bajeti imependekeza ongezeko la faini za makosa ya barabarani hasa yanayohusu mauaji ili kuzipunguza, akisema hiyo ni hatua nzuri.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya EY Tanzania, Joseph Sheffu, alisema bajeti hiyo ni shirikishi, lakini wasitegemee ilete mapinduzi kwa kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi.

“Kasi ya kufufua uchumi ni mchakato, kwa hiyo tunatakiwa kuwa makini kwa kuufanya uchumi kuwa endelevu,” alisema.

Alisema agenda ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu nishati safi ya kupikia imefanya bajeti hiyo kuwa kinara kupambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ambayo ni tishio kwa ukuaji uchumi.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Innocent Donald, alisema bajeti hiyo inalenga kuhusisha sekta binafsi kwenye maendeleo ya nchi.

Naye Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Buberwa Kaiza, alisema bajeti ameisoma na kubaina matumizi ya watawala ni mengi kuliko ya watu wa kawaida katika mambo ya maendeleo.

“Shughuli za watawala, posho, mishahara, kusafiri, mafuta inaonekana karibu nusu ya bajeti nzima ila sio jambo jema halifurahishi kwa watu walio wengi tungependa bajeti iwe sehemu kubwa ya fedha za serikali iende kwenye maeneo ambayo yanayogusa watu wengi kama kilimo,” alisema Kaiza.

Alisema sehemu ya fedha iende kwenye shughuli za nchi ambazo zinahusisha watu wengi kuna vijiji havina mawasiliano, hivyo vikiwezeshwa itasaidia mazao yanayozalishwa kujua soko lilipo.

Kaiza alisema inahitajika kutengwa kwa fedha za kuwawezesha wawekezaji katika kilimo kuongeza maghala ya kuhifadhi mazao na barabara za vijini kuwekwa lami ili kurahisha usafirashaji.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Maendeleo ya Jamii na Uchumi (REPOA), Dk. Donald Mmari, alisema bajeti hiyo imezingatia baadhi ya maoni, malalamiko na mahitaji ya wananchi.

“Katika maeneo hasa ya uzalishaji kwenye kilimo na kuangalia namna bora ya kuhamasisha, kupunguza uuzaji nje wa malighafi na kusisitza kuongeza thamani ndani ya nchi lakini pia kujaribu kupanua wigo wa ulipaji wa kodi yaani kuongeza walipa kodi wengi ili kupunguza mzigo kwa watu wanaolipa kodi,” alisema

Aidha, alisema kuongezeka kwa kiwango cha kuwalipa wastaafu imeongezeka kidogo kwa kuwa kuna uwekezaji wa fedha hizo unapaswa kuongeza thamani ya michango ya wanachama ili waweze kupata kipato ambacho baada ya kustaafu wapate kiasi kikubwa cha fedha zao.

“Fedha hizo wamekuwa wakizichanga na kuziwekeza kwa muda mrefu zimeongezeka na kuzaa mfumo wa usimamizi wa hizo taasisi zinazosimamia mifuko ya hifadhi ya jamii inapaswa kubadilika,” alisema.

IMEANDALIWA na Beatrice Shayo na Romana Mallya