Macha ‘acharuka’ ataka kuona thamani ya fedha

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 12:29 PM Apr 13 2024
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, akikagua mradi wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kishapu.
Picha: Marco Maduhu
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, akikagua mradi wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kishapu.

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, aonyesha kutofurahia usimamizi wa fedha za miradi ya maendeleo. baada ya kuona mapungufu katika jengo la ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, na hivyo kuamuru kufanyika kwa marekebisho, sambamba na kuwataka watumishi wa umma wilayani humo kuhakikisha thamani ya fedha katika miradi inaonekana.

RC Macha amebainisha hayo pale alipofanya ziara wilayani Kishapu na kisha kuzungumza na watumishi wa umma  pamoja na kukagua baadhi ya miradi ya maendeleo, sambamba na kulikagua Jengo la ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo, ambapo alibaini mapangufu  kama milango kuwa chini ya kiwango.

"Jengo la ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kishapu ni zuri, lakini kuna dosari kwenye uwekwaji wa milango, kwani ipo chini ya kiwango. Niwatake wanaosimamia ujenzi wa jengo hili, kusimamia vyema ili liwe na kiwango kizuri, pamoja na kufanyiwa marekebisho ya milango," amesema na kuongeza;

“Wahandisi wa Serikali kuweni Wazalendo na nchi yenu pamoja na Watumishi wote, simamieni vyema fedha hizi za miradi ya maendeleo, ili miradi iwe ya kiwango bora na kuonekana thamani ya fedha."

RC Macha aliendelea kusema: “Pia naagiza jengo hili likamilike kwa wakati ambapo mmeniambia limefikia asilimia 95; na kwamba June 30, litakuwa tayari, nitakuja hapa kulifungua sasa nikute bado halijakamilika."

Aidha amewataka watumishi wilayani humo, kuheshimiana kila mmoja kwa nafasi yake, pamoja na kuacha kujiingiza kwenye mahusiano ya kimapenzi, ambayo mara nyingi yamekuwa yakivuruga ufanisi wa utendaji kazi.

Katika hatua nyingine RC Macha, amezungumza na Wazee wilayani humo, na kuwahakikishia Serikali itaendelea kuwatunza pamoja na kuwapatia huduma mbalimbali zikiwamo matibabu na upatikanaji wa dawa kwa wazee hao.

Awali Kaimu Katibu Tawala Wilaya ya Kishapu, Fadhili Mvanga, akisoma taarifa kwa mkuu huyo wa mkoa juu ya ujenzi wa jengo hilo, amesema lilianza kujengwa Marchi mwaka 2022, na linatarajiwa kukamilika June 30, mwaka huu na gharama zake ni Sh.bilioni 1.6.