Mabula aomba radhi madai wagonjwa kulala wodi moja

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 10:56 AM Sep 05 2024
MBUNGE  wa Ilemela (CCM), Dk. Angelina Mabula
Picha: Mtandao
MBUNGE wa Ilemela (CCM), Dk. Angelina Mabula

MBUNGE wa Ilemela (CCM), Dk. Angelina Mabula, ameomba radhi bungeni na kufuta maneno yake kwamba wagonjwa wanaume, wanawake na watoto wanalazwa kwenye wodi moja katika Kituo cha Afya Sangabuye mkoani Mwanza.

Mabula amefikia hatua hiyo baada ya ushahidi wake aliowasilisha bungeni kuonesha kuwa jambo alilolisema si la kweli licha ya kituo hicho kukabiliwa na uhaba wa  miundombinu. 

Waziri huyo wa zamani wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, aliomba radhi juzi bungeni kabla ya Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, kuahirisha kikao cha Bunge. 

“Asante Mheshimiwa Spika (Dk Tulia Ackson) kwa kunipa fursa kusema maneno machache baada ya kutoa maelezo namna ulivyopitia ushahidi wote ulioletwa. Pamoja na maelezo uliosema utambuzi ni kwamba bado pana changamoto na bado pale wamezungumzia wanapozidi bado wanaingia kule.

 “Kwa hiyo kama ilileta mtafaruku kwa namna ambavyo hali halisi nilivyoiwasilisha, Mheshimiwa Spika naomba kufuta hayo maneno lakini changamoto inabaki ile ile ya kwamba hakuna miundombinu na naomba radhi kama limeleta mtafaruku katika kuelewa hoja halisi niliyokuwa nimeileta,” alisema Mabula. 

Awali, Spika Tulia alisema: “Mtakumbuka Agosti 27, 2024 wakati wa maswali na majibu, Mheshimiwa Mabula alipata fursa ya kuuliza swali la nyongeza na aliuliza Kituo cha Afya cha Sangabuye kilipandishwa hadhi 1999 kutoka zahanati na kuwa kituo cha afya. Kituo hicho hadi leo kina wodi moja ambayo inatumika na wanawake, wanaume  na watoto na kuhoji serikali lini itakamilisha miundombinu ikiwa ni pamoja na kujenga uzio.”

Baada ya swali hilo, Spika kabla ya kumpa nafasi Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dk. Festo Dugange, kujibu alimhoji mbunge ni kwa namna gani wanawake, wanaume na watoto wanalala wodi moja, hata hivyo  mbunge alisema hiyo ndiyo hali halisi iliyopo.

Naibu Waziri Dugange alisema hilo jambo katika hali ya kawaida haliruhusiwi na kuahidi kufuatilia ili kujua nini kinachoendelea huko.

Kutokana na uzito wa jambo hilo, Spika huyo alielekeza Naibu Waziri Dugange akimaliza kujibu maswali, aende kufuatilia jambo hilo na kumpa taarifa.

Kwa mujibu wa Spika Tulia, kabla ya kuahirisha Bunge, Naibu Waziri huyo aliwasilisha ushahidi wa maelezo na picha ya hali halisi ya kituo hicho na alimpa taarifa mbunge kuhusu maelezo hayo ya serikali ambayo yalibainisha kuwa kituo hakina wodi lakini watumishi wamejiongeza wameweka sehemu tatu za kulaza wagonjwa.

“Ile taarifa ilionesha kuwa wodi hakuna isipokuwa vyumba ambavyo vingetumika kwa ajili ya shughuli nyingine hapo vinatumika kwa ajili hiyo wakati wa kusubiri ujenzi wa wodi. Mheshimiwa Mabula alisimama na kuomba mwongozo kuwa yale maelezo yaliyotolewa kama ushahidi hakuna uhalisia kwa kuwa yeye amefanya ziara kwenye hilo eneo hivi karibuni na kukuta wanawake, wanaume na watoto wanalala sehemu moja,” alisema.

Spika Tulia alisema alimhoji mbunge huyo kama ushahidi uliotolewa ni uongo na alisimamia msimamo wake kuwa maelezo aliyotoa ndio uhalisia ulioko kituoni hapo na kumtaka awasilishe Ushahidi unaothibitisha jambo hilo.

“Ushahidi tumeupitia ambao mmoja ni kutoka ofisi ya mbunge, mwingine unatokana na kikao cha kamati ya siasa cha kata ya Sangabuye ambao unaonesha wakati wakijadili jambo hilo maelezo yaliyochukuliwa mjadala uliashiria kwamba wodi ya wanaume hakuna. Wakati mwingine wakizidi wanahamishiwa chumba cha wanawake. Zile siyo wodi, vimetengwa vyumba tu vya kuhudumia wagonjwa na hawalazwi wote kwa pamoja,” alisema.

Alisema katika kuchambua ushahidi alichosema mbunge, kituo cha afya kina changamoto ya miundombinu ni kweli lakini hoja ya wagonjwa kulala pamoja si kweli.