Kikwete: Niliishi na Lowassa hivi

By Elizabeth Zaya ,, Godfrey Mushi ,, Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 11:47 AM Feb 13 2024
Rais Mstaafu, Jakaya Mrishio Kikwete akisaini kitabu cha maombolezo katika msiba wa aliyekuwa Waziri Mkuu Msaidizi Edward Lowassa.
PICHA :Na CCM
Rais Mstaafu, Jakaya Mrishio Kikwete akisaini kitabu cha maombolezo katika msiba wa aliyekuwa Waziri Mkuu Msaidizi Edward Lowassa.

RAIS mstaafu Jakaya Kikwete jana alifika kwenye msiba wa Waziri Mkuu wake wa kwanza, Edward Lowassa, akifunguka 'ya kabatini' maisha yao ya ofisini na uswahiba wao.

"Ninamfahamu marehemu (Lowassa) kwa muda mrefu, tulikuwa vijana pamoja, tulikuwa chuo kikuu (UDSM) pamoja, nilimtangulia mimi mwaka mmoja," alitamka Kikwete kwa sauti ya utashi.

Lowassa aliyefariki dunia Jumamosi iliyopita, alikuwa sehemu ya safu iliyompambania Kikwete kwa mara ya kwanza katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 na ule wa 2005 uliomweka madarakani.

Kwa mujibu wa Kikwete, Lowassa ni sehemu ya 'mabwana mipango' watatu waliomshawishi kuwania nafasi ya wadhifa ambao leo unampa hadhi Rais mstaafu.

"Ninamfahamu marehemu (Lowassa) kwa muda mrefu, tulikuwa vijana pamoja, tulikuwa chuo kikuu (UDSM) pamoja, nilimtangulia mimi mwaka mmoja," alitamka Kikwete kwa sauti ya utashi, akiendelea:

"Tulitangulia sisi kuingia kwenye chama (TANU) na baadaye yeye akafuata. Tumefanya kazi wote kwenye chama kwa muda wote, mimi nikaendelea na shughuli za jeshi (JWTZ) na baadaye tena nikarudi kwenye chama.

"Mwenzangu aliendelea moja kwa moja kwenye shughuli za chama, baadaye akawa mbunge na mimi baadaye nikateuliwa kuwa mbunge, naibu waziri. Kwa hiyo, tukawa wote kwenye harakati za kisiasa."

Akiwa ameambatana na mkewe, Salma, Kikwete pia alizungumzia misukosuko ya kisiasa iliyowagusa katika urafiki wao, akiitaja kuwa "ni changamoto kwenye maisha na haifuti mema na mazuri aliyolifanyia taifa". 

Lowassa alitumikia nafasi ya Waziri Mkuu katika zama za Kikwete kwa miaka miwili na miezi kadhaa kabla ya kujiuzulu na baadaye kuibukia kuwa mgombea urais kwa tiketi ya CHADEMA baada ya kukwama kuipata tiketi hiyo kwa kofia ya CCM mwaka 2015.

Kikwete alisimulia mkasa wa mwaka 1995, akiwa nyumbani kwake, alifuatwa na marafiki zake watatu wakiongozwa na aliyewahi kuwa Spika wa Bunge, Hayati Samuel Sitta, Lowassa na Rostam Aziz. Wakamshauri aende na rafiki yake (Lowassa) kuchukua fomu ya kuwania urais.

"Mwaka 1995, siku moja asubuhi, nikapokea ugeni, mtoto akaja chumbani, akaniambia 'baba kuna wageni'. Nikaenda chini nikakuta marafiki zangu watatu, kaka yangu Samwel Sitta, Edward Lowassa na Rostam Aziz. Wakaja kuniambia kwamba 'tunataka mwende na Edward Dodoma mkachukue fomu.

"Mimi nikasema 'jambo hilo halipo kwenye mawazo yangu', lakini mwenzangu lipo kwenye mawazo yake... nikasema 'basi mwacheni aende...' naye akasema 'na mimi siendi bila wewe'. Basi ikabaki ndiyo historia. 

"Tukabishana mpaka tukafika mahali tukakubaliana... 'basi wacha twende'. Kwahiyo, tukaenda tukachukua fomu zile tukazijaza, zikarudishwa... mchakato ndani ya chama... mwenzangu hakubahatika... mimi nikabahatika kuwamo katika wale watano.

"Na baadaye tukapigiwa kura kwenye NEC nikawamo kwenye wale watatu... kwenda mkutano mkuu... nikawamo katika wawili na tulivyobaki wawili kura zangu hazikutosha... akapata Mzee Mkapa... mimi nikaja kuwa Waziri wake wa Mambo ya Nje na mwenzangu (Lowassa) akaja kuwa waziri tena," alisimulia.

Kikwete alisema wakiwa wanatumikia nafasi hizo, waliendelea kuweka mikakati kwa ajili ya kugombea tena katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.

"Basi tumeendelea hivyo na kuweka mikakati ya pamoja ya mwaka 2005, tukateuliwa kugombea, mwenzangu akateuliwa kuwa Waziri Mkuu... akapata changamoto katikati, ikabidi akae pembeni... lakini tukaendelea kuwa pamoja, kuwa marafiki, tukishirikiana kwa kila linalowezekana.

"Ameugua, Mwenyezi Mungu ameichukua roho yake. Ninachoshauri tu tuendelee kumwombea, (Mungu) aipokee roho yake na aiweke mahala pema peponi. 

"Edward ametoa mchango mkubwa kwa taifa letu, yaliyotokea ni changamoto katika maisha, lakini hayafuti yale mema na mazuri aliyolifanyia taifa letu," alisema.

Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi alisema amepokea taarifa za kifo cha Lowassa kwa masikitiko makubwa kwa sababu walifanya naye kazi wakiwa mawaziri katika serikali ya awamu ya tatu.

Alisema amekwenda kutoa salamu za pole kwa familia ya marehemu kwa niaba ya wananchi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutambua mchango mkubwa wa kiongozi huyo kwa taifa.

WATAKA KITABU 

Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CHADEMA), Aida Khenani na Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, wameomba kiandikwe kitabu cha kumbukumbu ya Lowassa ili kumbukumbu nzuri kuhusu maisha yake ya uongozi na siasa zibaki kuwa funzo kwa viongozi na wanasiasa wengine nchini.

Wanasiasa hao walitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti wakati wakizungumzia milima na mabonde aliyopitia Lowassa.

Zitto alisema kitendo cha Lowassa kujiuzulu nafasi yake lilikuwa ni jambo kubwa ambalo linapaswa kuwa mfano kwa viongozi wengine pale inapowabidi kufanya hivyo.

"Lowassa alipata ajali ya kisiasa, ikatokea skendo kubwa tu ya Richmond, Kamati ya Bunge ikatoa taarifa na mimi nilikuwa bungeni siku ile, na yeye akaona kwamba ametajwa, na alisema siku ile kwamba ‘nimeonewa na sikupewa nafasi ya kusikilizwa, lakini inaonekana shida ni Uwaziri Mkuu’, akaachia nafasi hiyo.

"Ni hatua kubwa sana kwa sababu Waziri Mkuu, katika nchi yetu ni mtu wa tatu katika utendaji na uongozaji wa serikali na dola, na alikuwa mtu wa kwanza kuzungumza bungeni siku ile, na akamaliza mjadala kwa kujiuzulu na serikali nzima ikaanguka, Rais Kikwete akatafuta Waziri Mkuu mwingine, akaunda serikali," alisema Zitto.

Alisema licha ya Lowassa kuanguka kisiasa, baadaye aliibuka na kuwa mwanasiasa mkubwa na kila mtu akawa anataka kumwona na kuwa upande wake. Kumbukumbu hizo zote zinapaswa kuwekwa kwenye vitabu ili kubaki kuwa funzo.

"Ingekuwa ni nchi nyingine sasa hivi kungekuwa kuna vitabu kuhusiana na kuanguka na kusimama kwa Lowassa, lakini nchi yetu utamaduni ni mdogo, kulipaswa kuwa na utafiti wa kutazama hayo.

"Maana yake ninakumbuka mwaka 2008, Lowassa alikuwa akitembea anaweza kuzomewa, lakini miaka miwili baadaye kila mtu alitaka kuonana naye, kila mtu alitaka kuwa upande wake," alisema.

Zitto alikumbushia pia 'Safari ya Matumaini' aliyoianzisha Lowassa na namna 'ilivyosomba' watu.

"Kama kuna jambo ambalo ninaweza kujifunza kwa Lowassa ni uwezo wa kufanya uamuzi, lakini neno lingine kwa taifa na kwa Rais wa Jamhuri, lazima tufanye kitu cha kumthamini na kumkumbuka Lowassa," alisema.

Mbunge Khenani (CHADEMA) alisema Lowassa alionesha mfano wa kuigwa kwa kutanguliza maslahi ya taifa badala ya maslahi yake pale alipoonesha uthubutu na kujiuzulu.

"Kwenye uongozi ameacha alama yake, kama kiongozi lazima uoneshe mfano wa kuigwa, alionesha pamoja na kwamba alikuwa na nafasi kubwa ya Waziri Mkuu, akajiuzulu.

"Kwa wale ambao wanaweza kusaidia hasa familia yake, yale wanayoyajua na watu wa karibu wasaidie kuacha kumbukumbu halisi kwenye taifa letu kwa sababu wana alama yake," alisema mbunge huyo akikumbuka pia mchango wa Lowassa kwa CHADEMA kuchukua viti vingi vya ubunge na udiwani mwaka 2015.

STEVEN WASSIRA

Mwanasiasa mkongwe, Stephen Wassira alisema Lowassa alifanya kazi kubwa ndani ya CCM na serikali. Katika awamu ya tatu aliimarisha utoaji elimumsingi.

"Ninachoweza kuongea ni kwamba msiba wa ndugu yetu Edward Lowassa umetuondolea mtu muhimu sana ambaye alikuwa anatoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi yetu," alisema.

Aliwasihi Watanzania kuwa wakati wanaombeleza kifo cha kiongozi huyo wasikubali msiba wake uwagawe kichama au kitaifa, bali uwe kiungo cha kuwaunganisha na kuwafanya kuwa wamoja.

Mfanyabiashara Azim Dewji alisema Lowassa alikuwa kiongozi mwenye uchungu na nchi yake na kutaka watu wote wafahamu kuwa nchi ni yao na kufanya kazi kwa maslahi ya nchi.

PAUL MAKONDA

Katibu wa NEC (CCM) Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Paul Makonda, alisema alichojifunza kwa Lowassa ni ustahamilivu kwa kuwa katika maisha yake hajawahi kuinua kinywa chake na kujibu mapigo katika mapambano yote aliyoyapitia.

Aliwasihi Watanzania kumwenzi kiongozi huyo kwa kuiga mfano wa mema aliyoyatenda ikiwamo kutowekeana uhasama na visasi, bali washikamane na kuijenga nchi.

Makonda pia aliwataka watu kuacha kumzungumzia mtu kwa mazuri pale anapofariki dunia, akisisitiza wale ambao hawakwenda kumjulia hali wakati anaumwa, waache alichokiita unafiki kwa kujifanya kuwa ni rafiki yao.
 "Tuache unafiki kuna wengine wanajiita marafiki wa Lowassa na hawakwenda kumwona halafu baada ya kufariki dunia wanajifanya wao marafiki zake, lakini hawakujitokeza, waache kumsemea mtu mazuri baada ya kufa," alisema.

SHEIKH MKUU
 Sheikh Mkuu wa Tanzania, Dk. Abubakar Zubeir, aliwasihi wananchi kuendelea kumkumbuka kiongozi huyo kwa mazuri aliyoyafanya kwa taifa.

Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, akizungumzia maisha ya kisiasa ndani na nje ya CCM na utendaji wa Lowassa, alisema hakuwa kiongozi aliyekuwa anasema 'nenda uje kesho'.

LUHAGA MPINA

Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina, pia alimwelezea Lowassa kama Waziri Mkuu aliyekuwa na uamuzi mgumu, akitilia mkazo kuimarisha sekta ya elimu.

"Taifa limepata hasara kubwa ya kumpoteza aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa. Kwa kweli tutamkumbuka kwa mambo mengi. Moja ni uwezo mkubwa wa Lowassa katika kusimamia shughuli za serikali.

"Kile kilichopangwa kufanyika alikuwa na uwezo mkubwa sana wa kukisimamia na kukifuatilia. Wote mtakumbuka wakati tunaanza ujenzi wa shule za sekondari kila kata mwaka 2006, Lowassa akiwa Waziri Mkuu, alituita viongozi wa maeneo mbalimbali na kupewa maelekezo kwamba tunaanza ujenzi wa shule za kata na alisimamia hilo," alisema

NAIBU SPIKA 

Mussa Zungu, Naibu Spika alisema Lowassa alikuwa na uamuzi mgumu na alikuwa mkali, mcheshi na hakupenda kumwonea mtu wala kumdharau mtu.

Alisema wakati yeye akiwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Lowassa alikuwa Mwenyekiti wake, ndiko alikoanza kumjua vizuri, akaona uwezo, nguvu zake na ushawishi wake kwa mabalozi wa nchi mbalimbali.

“Huu ni msiba mkubwa sana kwa Watanzania wote. Mimi binafsi nimeguswa sana na msiba huu. Niliwahi kukutana na Lowassa katika zaira yake Mkoa wa Dar es Salaam, alivyokuja na ajenda za shule za kata, na yeye kipindi kile alikuwa na Waziri Mkuu na Waziri wa Elimu alikuwa Magreth Sitta. 

"Niliona namna alivyohangaikia shule zile, na kwa kweli shule hizi, ndio sasa zilizofaulisha watoto wetu, na vijana wengi wanapata division One (daraja la kwanza) kutoka shule zile," alisema.

Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Dar es Salaam, Mariam Kisangi, alisema Lowassa atakumbukwa kwa kuacha alama ya kudumu katika sekta ya elimu nchini, hasa pale alipotafuta mwarobaini wa changamoto kubwa ya watoto waliofaulu darasa la saba kukosa madarasa ya kusomea kidato cha kwanza.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka alisema Lowassa alikuwa mwanasiasa na kiongozi mwenye kishindo.

"Ninaweza kusema ulikuwa tembo wa siasa za CCM, kwa kauli na matendo ulibeba haiba ya kiongozi mwenye maono, matamanio na uamuzi wenye matokeo. Alama ya kazi zako kwa taifa lako pendwa la Tanzania hazihitaji tochi," alisema.