Kaya 74 zilizokumbwa na mafuriko ya Hanang' kukabidhiwa Nyumba Juni

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:40 PM May 30 2024
Ujenzi wa nyumba ukiendelea.

KAYA 74 za waathirika wa maporomoko ya tope na mawe kutoka mlima Hanang' zinatarajia kuhamia kwenye nyumba mpya walizojengewa na serikali.

Kaya hizo ni kati ya 108 zilizokosa makazi kutokana na maporomoko ya tope na udongo yaliyotokea  wilayani humo Desemba 3, mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 89.

Mkuu wa Wilaya ya Hanang' Almishi Issa Hazali  ameyasema hayo leo wilayani humo, alipotembelea na kukaguzi ujenzi wa nyumba 108 zinazojengwa katika kijiji cha Wareti.

Almashi aliwatembeza wataalam kutoka Wizara za Afya, Elimu, Maendeleo ya Jamii  na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) waliofika wilayani humo kufuatilia maisha ya waathirika wa janga hilo ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu ya afya ya akili na kuwajenga kisaikoljia wanafunzi mashuleni.

Amesema nyumba 74 zipo hatua ya mwisho ya kukamilika kwake na mwezi wa sita wanatarajia kaya 74 zitahamia na kukabidhiwa rasmi hati zao.