JWTZ, Jeshi la Ukombozi la China kufanya mazoezi ya pamoja nchini

By Restuta James , Nipashe
Published at 04:25 PM Jul 25 2024
JWTZ, Jeshi la Ukombozi la China kufanya mazoezi ya pamoja nchini.
Picha: Mpigapicha Wetu
JWTZ, Jeshi la Ukombozi la China kufanya mazoezi ya pamoja nchini.

MELI vita tatu za Jeshi la Ukombozi la watu wa China zimepokelewa nchini jana kwa ajili ya kuungana na vikosi vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), katika mazoezi ya kubadilishana uzoefu ili kuimarisha uhusiano wa miaka 60 ya ushirikiano wa nchi hizo mbili.

Akizungumza na waandishi wa habari katika mapokezi ya meli hizo, Kamanda wa Jeshi la Wanamaji (Navy), Rear Admiral Ameir Ramadhani Hassan, amesema meli hizo zimekuja nchini kwa ajili ya kufanya mazoezi ya kijeshi ya pamoja kati ya vikosi vya JWTZ na Jeshi la Ukombozi kwa lengo la kubadilishana uzoefu.

“Majeshi yetu yalishafanya mazoezi zaidi ya mara tatu katika kozi maalum lakini zoezi la mwaka huu ni kubwa zaidi kwa sababu linahusisha vikosi vya Jeshi la Anga (Air Force), Nchi Kavu (Land Force) na Wanamaji (Navy), jana tumeiaga Meli Vita Matibabu, baada ya kutoa huduma ya matibabu kwa Watanzania na imeondoka, leo tumepokea hizi," amesema Rear Admiral Hassan.

Amesema mbali ya kubadilishana uzoefu, wanajeshi wa pande zote watapata fursa ya kujifunza ujuzi wa kijeshi mpya kutoka kwa wenzao na kuimarisha uhusiano kati yao.

1
Amesema JWTZ imepeleka askari na maofisa wake nchini China, kwa ajili ya masomo mbalimbali ya kijeshi na kwamba ushirikiano huo unatimiza miaka 60 tangu kuanzishwa na Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, anauendeleza.

Kamanda Hassan amesema mazoezi hayo yanakwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 60 ya JWTZ ambayo kilele chake ni Septemba Mosi, mwaka huu.

Naye Kapteni Mwandamizi wa Jeshi la Ukombozi, Li Bo amesema wamefika nchini Tanzania kubadilishana mbiu na uzoefu wa kijeshi na JWTZ na kwamba ana imani watajijenga na kuwa imara kwa pamoja.