CHUO cha Uhasibu Arusha (IAA), kimetangaza mpango wa kufungua kampasi mpya nje ya nchi, moja katika Visiwa vya Comoro na nyingine Sudan Kusini , kufuatia mahitaji makubwa ya elimu ya juu na fursa za maendeleo katika maeneo hayo.
Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Eliamani Sedoyeka, ameeleza mpango huo, wakati wa kikao na wahariri wa vyombo vya habari kilichofanyika leo katika ukumbi wa chuo hicho jijini Arusha.
Profesa Sedoyeka amesema kuwa, hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kukifanya chuo hicho kuwa taasisi ya kimataifa inayotoa huduma bora za elimu kwa kukidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.
Amesema wamelenga kukimataifisha chuo hicho kwa kigezo cha kuandaa mitaala inayoendana na soko la ndani na nje ya nchi, teknolojia za kufundishia, kujifunzia kwa njia ya mitandao.
"Mpango huu unalenga kuboresha upatikanaji wa elimu ya juu na kuimarisha nafasi ya IAA katika kutoa mchango wa kielimu ndani na nje ya mipaka ya Tanzania," tumejipima tunakidhi vigezo vya kufanya hivyo,” amesema Profesa Sedoyeka.
Amesema IAA, kimejipambanua kwa ubora katika mafunzo ya uhasibu, biashara, tehama, fedha , utalii na ukarimu kulingana na mahitaji ya soko na kufungua kampasi mpya kwenye mikoa ya Dodoma, Manyara na Ruvuma ili kuongeza wigo wa huduma zake.
Prof. Sedoyeka, amesema kwa sasa chuo kina watumishi 370, kati yao 32 ni wenye Shahada ya Uzamivu na wanatarajiwa kufikia 100 baada ya wengine 88 kumaliza masomo yao.
Ameongeza kuwa mwaka 2025, chuo hicho kinatarajiwa kuwa na wanafunzi 20,000 idadi ambayo itakifanya kuwa miongoni mwa vyuo vikuu vyenye idadi kubwa ya wanafunzi nchini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED