MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama mkoani Singida,Asia Messos amewataka wakazi wa kata za Nkalakala na Miganga wilayani humo kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi wa Serikali Za Mitaa unaotarajia kufanyika Novemba 27, 2024.
Alitoa wito huo jana wakati wa ziara yake ya kikazi ya kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa kata hizo wilayani hapa.
“Mwaka huu tutakuwa na zoezi kubwa la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27,2024, tujitokeze kwa wingi wetu tushiriki uchaguzi huu kwa maendeleo ya kata zetu,usikubali mtu mwingine akuchagulie kiongozi wakati unauwezo wa kupiga kura,” alisema.
Messos alisema kuwa ili mwananchi aweze kupiga kura siku ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, anapaswa kujiandikisha katika daftari la orodha ya wapiga kura ambapo zoezi la uandikishaji litafanyika kuanzia Octoba 11 hadi 20, 2024.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED