CWT: Tusingependa kuwa na ‘stress’ sababu kufundisha

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 11:56 AM Feb 13 2025
Makamu wa Rais wa CWT Taifa, Suleiman Ikomba
Picha: Mtandao
Makamu wa Rais wa CWT Taifa, Suleiman Ikomba

CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT), kimeitaka serikali kuwachukulia hatua ama kuwaondoka katika nafasi zao watumishi wanaoshughulikia maslahi ya walimu, kwa sababu wameshindwa kutenda kazi zao vizuri na kusababisha walimu kuwa na msongo wa mawazo.

Makamu wa Rais wa CWT Taifa, Suleiman Ikomba, ametoa tamko hilo jana, wakati wa mkutano wa kutatua changamoto za walimu wa Mkoa wa Singida katika kliniki ya ‘Samia Teachers Mobile Clinic’.

Kliniki hiyo iliyoratibiwa na CWT kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Utumishi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Elimu na Tume ya Utumishi Tanzania huku mamia ya walimu kutoka halmashauri saba za Mkoa wa Singida wakifika kuwasilisha madai yao ambayo wanadai kwa muda mrefu.

“Hawa watumishi ambao wanashughulika na maslahi yetu walimu tumejikuta wanatusumbua sana, tunaomba wanaotusumbua waache kutusumbua kwa sababu mwisho wa siku tunataka tuanze kuchukua hatua, kwa mtu kwa jina sio kwa kuichafua serikali,” alisema.

Ikomba alisema walimu hawana nia mbaya ya kuisema vibaya serikali, lakini maofisa ambao wanashughulika na maslahi ya walimu washauriwe watende kazi vizuri na kama hawawezi kubailika waondolewe, kwa sababu wananababisha maumivu kwa walimu.

“Tumekutana na watendaji ambao wanatoa visingizio Mwalimu akifika ofisini kwao wanasema masuala yake walishayapeleka makao makuu utumishi, kumbe hawajafanya hivyo anadanganya tu, watumishi wa namna hiyo wanatusumbua walimu,” alisema.

Ikomba alisema haiwezekani mwalimu anafundisha watoto 100 darasani, halafu anawaacha kwa muda wa wiki nzima, ili kwenda Dodoma kufuatilia maslahi yake hivyo anayesabaisha matatizo ya namna hiyo, anatakiwa achukuliwe hatua.

“Walimu hawa leo, wanashughulikiwa na mimi nashukru wewe RC (Mkuu wa Mkoa) upo hapa nataka kuamini tukifika kwenye tathmini na kujua shida gani imetokea na nani amesababisha tusaidie kupunguza watu wawili wawili, ambao wanatusumbua walimu tushindwe kutekeleza shughuli zetu,” alisema. 

“Upo msemo unasema kwenye msafara wa mamba na kenge wapo sasa tunataka kenge waondolewe, ili wasiendelee kutusumbua katika utumishi wetu wa ualimu,” alisema.

Ikomba aliongeza kuwa walimu ambao wanafanya kazi ya kulea taifa hilo, kupitia watoto na vijana wasingependa kuwa na ‘stress’ kwa sababu  kazi ya kufundisha inataka utulivu..

Aliongeza kuwa wapo baadhi ya watu wanataka kuivuruga CWT, wakati taratibu zipo kisheria, lakini ama ni dalili ya rushwa au ni kutoelewa sheria wanachukua kama huruma .

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, alisema fursa ya kusikiliza na kutatua changamoto za walimu itakuwa mwendelezo kwa mkoa, ili na wao wafurahie maisha kama ilivyo kwa watumishi wengine.

Baadhi ya walimu walioshiriki kliniki hiyo, walisema changamo zinazowakabili ni madai ya malimbikizo ya mishahara, likizo bila malipo na kupewa uhamisho bila kulipwa madai ambayo wamekuwa wakidai kwa muda mrefu, bila kuopatiwa ufumbuzi.