CHINA imeikabidhi Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), vifaatiba mbalimbali vyenye thamani ya Sh. milioni 125, ikiwamo maalumu kwa ajili ya kukuza uoni wa mishipa ya damu na fahamu wakati wa upasuaji.
Balozi wa China nchini, Chen Mingjian, alikabidhi vifaa hivyo kwa Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, hospitalini hapo, kwa niaba ya Serikali ya Watu wa China, mwishoni mwa wiki, jijini Dar es Salaam.
Mhagama akizungumza baada ya kupokea msaada huo, alisema ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya ushirikiano kati ya Tanzania na China, kwenye sekta ya afya.
Alisema vifaa hivyo vitaisaidia MNH, kuboresha huduma za afya na kukabiliana na changamoto mbalimbali katika utoaji wa huduma za afya bora kwa wananchi.
“Ushirikiano kati ya nchi hizi mbili utaendelea kuwa na manufaa zaidi kwa pande zote, ikiwamo kuleta wataalam wa afya mabingwa wabobezi, vifaa vya kisasa vinavyotumia teknolojia ya hali ya juu ili kuongeza ubora wa huduma.
“Naupongeza uongozi wa MNH, kwa kuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa ushirikiano huu. msaada huu utachangia katika kuboresha utoaji wa huduma za afya na kutoa matokeo chanya kwa wananchi”, alisema Mhagama.
Balozi wa China nchini, Mingjian, aliishukuru Wizara ya Afya, MNH pamoja na timu ya madaktari kutoka China waliopo Tanzania, kwa michango yao muhimu katika ushirikiano wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili katika sekta ya afya.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Mohamed Janabi, aliishukuru China kwa msaada huo na kuomba ushirikiano zaidi katika maendeleo ya rasilimali watu na utoaji wa teknolojia za kisasa.
"Ushirikiano huu ni fursa kwa madaktari wetu kupata mafunzo ya ubingwa nchini China ambayo yataboresha ujuzi wao na kuwafundisha teknolojia na mbinu za kisasa hasa kwenye AI (akili mnemba), zinazohitajika katika huduma za afya," alisisitiza Prof. Janabi.
Alisema miongoni mwa vifaa vilivyokabidhiwa vitasaidia daktari awapo chumba cha upasuaji kuona kwa ukubwa mishipa myembamba ya damu na fahamu, kwa kutumia kifaa maalumu chenye darubini, ambacho huvaliwa kama miwani.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED