Abiria 1,400 wasafiri bure treni vya SGR, wafurahia kutumia muda mfupi

By Christina Haule , Nipashe
Published at 07:56 AM Jun 15 2024
Treni ya SGR.
Picha: Mtandao
Treni ya SGR.

ZAIDI ya abiria 1,400 wamesafirishwa bila malipo kwa treni ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro na kisha kurejea huku wakifurahia kutumia muda mfupi.

Ujenzi wa reli hiyo inayoaminika ni ndefu kwa Afrika yenye kilometa 300 ya kisasa itawezesha abiria kusafiri kwa gharama nafuu.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, ambaye alikuwa miongoni mwa wasafiri wa treni jana, alisema baada ya kuwasili kwenye kituo cha Morogoro kuwa treni hiyo imetumia saa 1:45 baada ya kutoka Dar es Salaam saa 12:10 na kufika Morogoro saa 1:55 asubuhi.

 â€śHili ni jambo la kihistoria na kutokana na furaha hii, wakati tunatoka Dar es Salaam Rais Samia Suluhu Hassan, ametuelekeza na Mkurugenzi ameanza kulitekeleza.

“Wale watakaosafiri leo (jana) kama ishara ya kusherekea ameelekeza watapanda bure kwa hiyo waliopanda kutoka Dar es Salaam kuja Morogoro na kurudi Dar es Salaaam amelipia yeye nauli kama shukrani,” alisema.

Kihenzile alisema kwa mara ya kwanza Tanzania imeanza safari za treni hiyo ya kisasa ambapo awali watanzania walitegemea treni za TAZARA pekee ambayo ina kilometa 1400 kutoka Dar es Salaam hadi Kapilimposh.

Alisema kwa Afrika, Tanzania ndio nchi pekee ambayo inajenga reli ndefu zaidi ya kisasa ambapo kwa kimataifa nchi kama China wana takribani kama kilometa 40,000, Hispania kilometa 3900, Japani kilometa 3700 na Ufaransa kilometa 2700 ambapo inayofuatia Tanzania ikishika nafasi ya tano,” alisema.

Aidha, alisema Tanzania ndiyo nchi pekee kwa Afrika iliyojenga reli ndefu ya kisasa na ya gharama nafuu ambayo inafungua uchumi kati ya nchi na nchi inazopakana nazo.

“Reli hii ni faida kwa wananchi wetu kutoka Dar es Salaam treni hii waliyokuja nayo ni Sh. 13,000 ambayo mwananchi wa kawaida anaiweza na kwenda mpaka Dodoma ni Sh. 30,000 na mwananchi anaweza kuwahi na akaenda kufanya shughuli zake na kurudi alipotoka,” alisema Kihenzile.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, alisema Watanzania wengi walilisubiri jambo hilo kwa hamu.

Kadogosa alisema watanzania wana haki ya kujivunia kwa kuwa inawezekana wakayaona ya kawaida, lakini si mambo ambayo yanatokea katika nchi zingine.

Alisema wananchi wananafasi kubwa ya kutumia reli hiyo katika shughuli za maendeleo ili kukuza uchumi wao na taifa kwa ujumla.  

Kadogosa alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza ahadi yake aliyoitoa bungeni ya kumalizia mradi wa ujenzi wa reli hiyo ikiwa ni sehemu ya miradi aliyoikuta wakati akiingia madarakani ikiwa chini ya asilimia 50.

“Alichokifanya Rais Samia ni kukamilisha ahadi za utekelezaji wa miradi na kitendo hicho ni kumuenzi mtangulizi wake, Hayati Dk. John Pombe Magufuli, kama kazi aliyoanzisha ameikamilisha kama alivyowaahidi Watanzania,” alisema.

Kadogosa alisema treni hiyo yenye mabehewa ya kawaida na kibiashara ina mabehewa 14.

Mwenyekiti wa Bodi ya TRC, Ally Karavina, aliwaomba watanzania kuzingatia muda wakati wa kupata huduma hiyo kwa kuwa inakwenda na muda uliopangwa tofauti na usafiri mwingine ikiwamo treni iliyozoeleka ya reli ya kati.

Alisema shirika linaweza kuongeza treni nyingine kulingana na mahitaji ya soko kwa kuwa na treni zinazokwenda Dar es Salaam na nyingine zinarudi Morogoro zikipishana ambapo abiria watapata huduma za kisasa.

Inda Mhando, ambaye alikuwa mmoja wa abiria  katika treni hiyo, alisema usafiri huo umemwamasisha kusafiri zaidi kwa kuwa ni moja pia ya utalii wa ndani.

Naye Mohamed Khasim, alisema usafiri huo akilinganisha na mabasi, unaokoa muda wa msafiri kwa kufika haraka.

Ujenzi wa reli hiyo ya kisasa ulianza rasmi Aprili, 2017 na katika awamu ya kwanza, umekamilika kipande cha Dar es Salaam - Morogoro na awamu ya pili, Morogoro hadi  Dodoma na awamu zingine ziko katika hatua mbalimbali za ujenzi ikiwamo Dodoma (Makutopora) - Tabora, Tabora- Isaka na Isaka-Mwanza.