Miili 300 yabainika kwenye kaburi la pamoja

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:17 AM Apr 23 2024
Miili 300 yabainika kwenye kaburi la pamoja.
PICHA: CNN
Miili 300 yabainika kwenye kaburi la pamoja.

WAFANYAKAZI wa Ulinzi wa raia wamegundua kaburi la pamoja lenye takriban miili 300 na kulifukua katika hospitali ya Nasser kusini mwa Gaza na baada ya kuondoka kwa vikosi vya Israel katika eneo hilo Aprili 7, mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Ulinzi wa Raia wa Khan Younis huko Gaza, waliipata miili hiyo ya mashahidi kutoka kwenye kaburi la umati katika uwanja wa hospitali ya Nasser Medical Complex tangu kuondoka kwa jeshi la Israel katika ukanda huo.

Imeelezwa kuwa mji wa Khan Younis umeachwa katika hali mbaya huku makazi ya wananchi yakibakia magofu baada ya mashambulizi ya miezi kadhaa ya Israel.

Mkurugenzi huyo wa ulinzi wa raia alietambulishwa kwa jina moja Suleiman alidai kuwa baadhi ya miili hiyo ilipatikana ikiwa imefungwa mikono na miguu.

"Kulikuwa na dalili za kunyongwa shambani, hatujui kama walizikwa wakiwa hai au waliuawa. Miili mingi imeharibika," amesema.

Mwanaume mmoja katika eneo la tukio aliambia CNN kwamba bado hajapata mwili wa mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka 21, ambaye aliuawa Januari mwaka huu.

“Bado sijampata, tulikuwa tumemzika kule. Lakini hatuwezi kumpata, na tulitaka kumfanyia kaburi la heshima,” amesema.

CNN