TAASISI ya Viwango Zanzibar (ZBS) imesema inaendelea na miradi ya ujenzi wa maabara tano za kisasa za ukaguzi ikiwamo ofisi na maabara inayojengwa Chamanangwe, Pemba ili kuongeza ufanisi.
Mkurugenzi Mkuu wa ZBS, Yussuph Majid Nassor, aliyasema hayo jana wakati akifungua Jukwaa la Vyombo vya Habari lililoandaliwa na taasisi hiyo kwa uratibu wa Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC) katika ofisi za makao makuu ya taasisi hiyo, Maruhubi, Mjini Unguja.
Alisema hatua hiyo imelenga kuongeza ufanisi wa taasisi kwenye ukaguzi, udhibiti na uthibitishaji wa viwango vya bidhaa zinazozalishwa na kuingizwa nchini kwa manufaa ya wananchi na mazingira.
Nassor alisema hatua hiyo itapunguza changamoto ya kusafirisha sampuli za bidhaa kutoka Pemba hadi Unguja kwa ajili ya uchunguzi na pia kupata majibu ya haraka. Alisema mradi huo utagharimu Sh. bilioni 6.5.
“Tayari zabuni za ujenzi zimeshatangazwa baada ya kukamilika kwa hatua za awali za ujenzi huo ikiwamo ya usanifu wa michoro. Ujenzi utakapoanza, utachukua miezi 24 hadi kukamilika, hivyo kupanua wigo wa utendaji,” alisema.
Kuhusu uimarishaji wa majukumu ya taasisi, alisema alisema imeendelea kuimarisha maabara za taasisi hiyo zilizozinduliwa mwaka jana pamoja na kukamilisha hatua za awali za kituo cha ukaguzi wa magari kitakachofunguliwa baadaye mwezi huu.
Pia alisema taasisi ina mradi wa kituo cha magari ambao umegharimu Sh. bilioni 2.5 umekamilika katika hatua ya majengo na wiki ijayo, ufungaji mitambo unatarajiwa kuanza.
Mbali na miradi ya ujenzi, alisema taasisi hiyo pia imepata mafanikio yakiwamo kutambuliwa kimataifa na Shirika la Viwango Duniani (ISO) na baadhi ya maabara zake kupata alama ya ithibati ubora ya mashirika ya kikanda likiwamo la ukanda wa Kusini mwa Afrika.
Makamu Mwenyekiti wa ZPC, Tabia Makame Mohammed, aliipongeza taasisi hiyo inavyofungamana na vyombo vya habari na kuomba taasisi zingine kuiga mfano huo.
Alisema vyombo vya habari ni daraja linanowakutanisha wananchi na taasisi za umma au binafsi hivyo wanapaswa kufanya kazi kwa pamoja.
Aidha, aliipongeza ZBS kwa kuendelea kupiga hatua za maendeleo ikiwamo kujitegemea kwa asilimia, 100 hivyo kuiondolea serikali mzigo wa uendeshaji jambo linalotokana na usimamizi bora wa ukusanyaji wa mapato na utoaji wa huduma bora.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED