Wizara Zanzibar, USAID washirikiana kukuza matumizi ya nishati mbadala

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:51 AM Jun 17 2024
Wizara ya Maji, Nishati na Madini kwa kushirikiana na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kupitia Mpango wa Power Africa, iliendesha warsha ya Nishati mbadala Zanzibar.
Picha: Ubalozi wa Marekani Tanzania
Wizara ya Maji, Nishati na Madini kwa kushirikiana na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kupitia Mpango wa Power Africa, iliendesha warsha ya Nishati mbadala Zanzibar.

WIZARA ya Maji, Nishati na Madini kwa kushirikiana na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kupitia Mpango wa Power Africa imeendesha mafunzo ya nishati mbadala Zanzibar.

Mafunzo hayo yamekutanisha wadau wa sekta ya utalii na kampuni binafsi za nishati kutokana na Shirika la Maendeleo la Kimataifa (USAID) kuunga mkono sekta ya utalii Zanzibar kwa kuhakikisha inaingiza mapato makubwa zaidi kwa uchumi.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Ubalozi wa Marekani nchini, lengo lingine ni kuhakikisha sekta hiyo inapata nishati ya uhakika kwa ajili ya hoteli na fukwe zinazopokea maelfu ya wageni kila mwaka.

Warsha hiyo ilitoa fursa za matumizi ya nishati mbadala kwa sekta ya utalii Zanzibar ikiunganisha hoteli na kampuni zinazotoa huduma za nishati mbadala. Pia kulikuwa na majadiliano na uwasilishwaji mada kuhusu matumizi ya nishati mbadala nje ya Gridi ya Taifa.

“USAID na Power Africa zinafurahishwa na ushirikiano wa Serikali ya Zanzibar katika kuhimiza umuhimu wa matumizi ya nishati mbadala kwenye sekta ya utalii,” alisema Plato Hieronimus, Naibu Mkurugenzi wa Ofisi ya Ukuaji wa Uchumi ya USAID/Tanzania. 

“Tuna matumaini kuwa majadiliano yaliyofanyika kwenye warsha hii yataleta matokeo chanya ambayo Zanzibar inaweza kuyatumia kuweka mazingira wezeshi kwa maendeleo,” aliongeza.

Taarifa hiyo ilibainisha kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pia imebainisha uzalishaji nishati mbadala kuwa muhimu kwa ukuaji wa sekta hiyo, kutegemea vyanzo vya nishati mbadala kutahakikishia usambazaji umeme thabiti na wa bei nafuu kwa hoteli, ambazo zinaweza kuongezwa au kupunguzwa matumizi kulingana na misimu, na hivyo kuokoa gharama na rasilimali.

“Tunafurahia matumizi ya nishati mbadala kama chanzo cha nishati inayotumika katika hoteli zetu na kukidhi mahitaji ya sekta ya utalii,” alisema Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Shahib Kaduara. 

“Matumizi ya nishati mbadala yatazifanya hoteli zetu kuwa na nguvu, mwanga na kufanya kazi, jambo ambalo litaimarisha sekta ya utalii na uchumi wa Zanzibar,” aliongeza.

Wakati dunia inashughulikia mahitaji ya nishati yanayoongezeka kila kukicha, pamoja na tishio la mabadiliko ya tabianchi, Zanzibar ina mikakati ya kufikia kujitegemea katika nishati kwa kuangalia fursa zinazopatikana kupitia nishati mbadala. USAID na Power Africa zinajivunia kukuza utumiaji wa vyanzo safi, vya bei nafuu na vya kutegemewa vya nishati.