Watakiwa kuwa mabalozi wa kilimo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:19 AM Jan 24 2025
Watakiwa kuwa mabalozi wa kilimo.
Picha: Mtandao
Watakiwa kuwa mabalozi wa kilimo.

VIJANA wametakiwa kuwa mabalozi wazuri wa mabadiliko katika sekta ya kilimo kwa kutumia teknolojia za kisasa ili kuweza kuzalisha kwa tija na kukuza uchumi wao.

Wito huo ulitolewa juzi na Mratibu wa Mradi wa YEFFA (Mechanization) chini ya AGRA, Fredi Kamande wakati wa mafunzo kwa vijana 61 kutoka wilaya za Njombe na Wanging’ombe yaliyofanyika Kata ya Ilembula wilayani hapa.

Kamande, alisema vijana hao wamepata mafunzo maalumu ya usimamizi wa zana za kilimo na ubunifu wa teknolojia za kilimo. 

“Mafunzo haya yalilenga kuboresha sekta ya kilimo kwa kuongeza tija na ufanisi kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa kwa vijana ili waweze kuingia kwenye kilimo wakiwa na ufahamu wa kutosha,” alisema.

Alisema hatua hiyo pia inalenga kuwawezesha kujiajiri na kupunguza changamoto za upatikanaji wa teknolojia za kilimo katika maeneo mbalimbali nchini. 

“Lengo letu ni kuwawezesha vijana hawa kuwa mabalozi wa mabadiliko katika sekta ya kilimo kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa,” alisema Kamande.

Alisema  YEFFA unasimamiwa na AGRA kwa ufadhili wa Mastercard Foundation ili    kuinua kilimo kupitia teknolojia bunifu. 

“Pia unawapatia vijana nafasi ya kuendeleza ujuzi wao na kujipatia ajira endelevu na hii inaendana na malengo ya serikali ya Tanzania ya kukuza sekta ya kilimo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030,” alisema. 

Awali Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, aliwataka wakulima mkoani humo kutumia teknolojia za kisasa kuongeza tija na ubora wa mazao yao. 

“Matumizi ya zana za kisasa za kilimo ni msingi wa mapinduzi ya kilimo. Wakulima wa Njombe wanapaswa kutumia teknolojia hizi ili kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi wa mkoa wetu,” alisema. 

Alisema Njombe unalenga kufikia malengo ya kitaifa ya kuboresha sekta ya kilimo na kuhakikisha vijana wanapata ujuzi na ajira katika teknolojia za kisasa za kilimo.

Mmoja wa wanufaika wa mradi huo, Franco Musha,  alisema vijana wengi wanaogopa kuingia kwenye kilimo kutokana na zana duni, hivyo kuwepo wa zana za kisasa utakuwa chachu kwa wengi kuingia kwenye sekta hiyo.