KATIKA kurahisisha huduma za kifedha kwa jamii, Kampuni ya simu ya Tigo imeungana na benki ya TCB kuendesha huduma kikoba kupitia Tigopesa.
Huduma hiyo mpya iliyozinduliwa jana jijini Dar es Salaam itawapa fursa wananchi kuwa na Uhuru wa kufungua, kujiunga na kuratibu vikoba mtandaoni.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Afisa Mkuu wa Tigopesa, Angelica Pesha, alisema huduma ya kikoba italeta suluhu ya changamoto za kifedha kwenye jamii.
"Huduma hii inawapa watumiaji usalama, uwazi zaidi kati yao, na uhakika wa kuratibu pesa zao kwa umakini zaidi huku kila mwanachama akiona kinachofanyika," alisema Angelica.
Aidha, alisema huduma hiyo itakua inafanyika kwa urahisi kupitia simu ya mkononi.
Kwa upande wake Mkuu wa Uwendeshaji wa TCB, James Msuya, alisema wamefurahi kuungana na tigo kuleta huduma hiyo muhimu kwa jamii.
"Kama benki tunajivunia kuwa sehemu ya kutatua changamoto za huduma za kifedha kwa wananchi, tunaamini huduma hii mpya inaenda kuwasaidia wananchi," alisema Msuya.
Alisema wataendelea kushirikiana na taasisi nyingine kuwasaidia wananchi kuwapatia huduma za kifedha wanazozihitaji.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED