WAKULIMA katika Halmashauri ya Mji wa Makambako mkoani Njombe wametakiwa kuachana na malalamiko kuhusu bei ya mazao na badala yake wazingatie maelekezo ya wataalamu, ili kupata tija katika kilimo chao.
Kauli hiyo imekuja baada ya wakulima walio wengi kuendelea kulalamikia kuhusu bei ndogo ya mazao wakati wanachozalisha hakina tija kutokana na kutumia eneo kubwa la shamba kuzalisha kiasi kidogo cha mazao, hivyo kushindwa kumudu gharama za uendeshaji
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Mji wa Makambako, Beatrice Tarimo wakati wa uzinduzi wa duka la pembejeo za kilimo One Acre Fund uliofanyika katika halmashauri hiyo wilayani Njombe.
Alisema wakulima walio wengi wamekuwa wakilalamikia bei ya mazao lakini changamoto kubwa iliyopo kwa Watanzania katika kilimo siyo bei bali ni tija katika kile kinachozalishwa.
“Uzalishaji kwa eneo mkulima anasema bei ya mazao ni ndogo kwa sababu kama kwenye ekari moja amevuna gunia nne akaenda kuziuza Sh. 30,000 maana yake atapata sh. 120,000 ukilinganisha gharama za uzalishaji na alichokipata hakiendani kwahiyo kwa haraka haraka mkulima atakwambia shida yetu kubwa ni bei ya mazao,” alisema Tarimo.
Tarimo alisema wakulima wanatakiwa kuondokana na tatizo la bei kwa kuanza kupambana na tatizo la tija katika kile ambacho kinazalishwa na wakulima.
Alisema katika kupambana na tatizo la tija wakulima wanatakiwa kupata pembejeo kwa wakati ikiwemo mbolea, mbegu pamoja na viwatilifu.
Hata hivyo Tarimo alisema ili kilimo kiwe endelevu wakulima wanatakiwa kuchukua hatua kwa kulima kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira.
Ofisa Kilimo kutoka kitengo cha pembejeo katika Halmashauri ya Mji wa Makambako, Peter Emmanuel alisema ili wakulima wapate tija ya kile wanachozalisha wanatakiwa kufuata kanuni za kilimo ikiwemo kuundaa shamba mapema kabla ya msimu wa kilimo kuanza.
Ofisa Uhusiano kutoka One Acre Limited Tanzania, Enhart Israel alisema uzinduzi wa duka hilo la pembejeo za kilimo utaleta chachu na kuongeza upatikanaji wa pembejeo za kilimo kwa urahisi.
Diwani wa Kata ya Kitisi, Halmashauri ya Mji Makambako, Navy Sanga alisema uzinduzi wa duka hilo la pembejeo limewasaidia wananchi wa kata hiyo ambao awali walilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo hadi Njombe Mjini.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED