WAFUGAJI wa samaki kwa njia ya vizimba wa Ziwa Victoria wamekiomba Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kutatua kero zao ili waweze kufanya uwekezaji katika mazingira rafiki na wezeshi.
Ombi hilo lilitolewa juzi wilayani hapa Mkoa wa Mwanza na Ofisa Rasilimali Watu na Utawala wa Kampuni ya Uwekezaji Samaki kwa njia ya vizimba ya Big Best, Simon Nzumbi wakati akiwasilisha kero zinazowakabili kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TIC, Dk. Binilith Mahenge.
Nzumbi, alizitaja baadhi ya kero hizo kuwa ni kukatika kwa umeme mara kwa mara, kuvamiwa kwa maeneo tengefu na wavuvi kisha kuvua samaki bila kibali na ufinyu wa maeneo ya kuchimba mabwawa ya kufugia samaki.
Nyingine ni chakula kwa ajili ya uzalishaji samaki kutoka nje ya nchi kuuzwa kwa gharama kubwa na kuchelewa kwa makontena ya vifaa vya mradi kutolewa bandarini licha ya mawakala kulipwa fedha zao kwa wakati.
“Pia tuna upungufu wa eneo la mita za mraba 20,000 umekuwa kikwazo katika matarajio yetu ya kuzalisha tani 900 hadi 1,200 za sato kwa mwezi ifikapo mwaka 2026,” alisema Nzumbi.
Alisema mpaka sasa, wamepandikiza vijiti 1,000,000 kwenye vizimba vikubwa na kuanza kuvunwa Julai mwaka huu baada ya samaki kukomaa.
Alisema wanatarajia kuwa na jumla ya vizimba na vizimba vitalu 200 kutoka 112 vya sasa ifikapo mwaka 2026.
Baada ya kupokea kero hizo, Dk. Mahenge, aliahidi watazifanyia kazi kwa kuwa uwekezaji huo wa samaki ni muhimu kwa Mkoa wa Mwanza na taifa.
Alisema wanatarajia uwekezaji huo utatengeneza ajira 400 nchini za muda mfupi na za kudumu, teknolojia na mtaji.
“Hili lingine la makontena naomba tulichukue wataalamu wangu wataliandikia taarifa tutawapelekea ofisini waone namna ya kufanya upokeaji wa mizigo ili liweze kuharakishwa,” alisema Mahenge na kusisitiza kuwa:
“Mimi naamini kama mmesajiliwa na TIC, mkitoa taarifa inaweza ikaharakishwa msiende peke yenu dawati letu litawasaidia.”
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED