Wachimbaji madini walia athari zebaki

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 09:37 AM May 10 2024
Wachimbaji wadogo wa dhahabu katika mgodi wa Mwakitolyo Nyaligongo wilayani Shinyanga.
Picha: Mtandaoni
Wachimbaji wadogo wa dhahabu katika mgodi wa Mwakitolyo Nyaligongo wilayani Shinyanga.

WACHIMBAJI wa dhahabu katika mgodi wa Mwakitolyo uliopo Kata ya Mwakitolyo wilayani Shinyanga, wameeleza athari ya matumizi ya kemikali ya zebaki wakati wakichenjua ikiwa ni pamoja na kupata ulemavu wa ngozi.

Walibainisha hayo juzi wakati wa mafunzo ya matumizi salama ya kemikali ya zebaki kwa wachimbaji wadogo na wasambazaji, iliyokuwa yanatolewa na Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Ofisi ya Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Mmoja wa wachimbaji hao, Juma Daudi alisema ukosefu wa elimu juu ya matumizi salama ya kemikali ya zebaki inasababisha wengi wao kupata madhara ambayo hayana tiba kutokana na kufanya shughuli hizo bila kuchukua tahadhari yoyote.

Mchimbaji mwingine Charles Misalaba alisema yeye ni miongoni mwa waathirika wa kemikali ya zebaki, kwamba amekuwa mtu wa kupoteza kumbukumbu kuwa na hasira muda wote na kuwa na msongo wa mawazo.

Hivyo aliiomba serikali kuangalia namna ya kumsaidia kupata tiba yake ili kuondokana na adha hiyo.

 Meneja wa Ukaguzi na Usajili kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Dodoma, Magdalena Mtenga, alisema kunakiwango cha zebaki kinachoruhusiwa kuwa mwilini ila kinapozidi unatakiwa kuacha shughuli za uchenjuaji na kufanyakazi nyingine kwani tatizo hilo halina dawa.

Hata hivyo alibainisha kuwa baadhi ya madhara yanayowapata wachimbaji pindi wasipochukua tahadhari kuwa ni pamoja na kuathirika kwa mfumo wa fahamu, figo, uwezo wa kuona, mikono kutetemeka, mimba kutoka, watoto kuzaliwa na utindio wa ubongo na kuchanganyikiwa.

Awali Ofisa Ufuatiliaji na Tathmini wa mradi huo kutoka NEMC, Hassan Maalim alisema wanatekeleza mradi wa kudhibiti matumizi ya zebaki kwa wachimbaji ili waweze kuwa na mazingira yenye viwango vinavyohitajika kwa mujibu wa mkataba wa Minamata.

Alisema mradi huo wanautekeleza katika mikoa ya Geita, Mbeya, Singida, Mwanza, Mara, Songwe na Shinyanga kwa sababu wengi wao wanafanya kazi katika mazingira magumu bila kuchukua tahadhari yoyote.