Vijiji vyapokea boti kukabili uvuvi haramu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:36 PM Jan 29 2025
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Matilda Buriani (watatu kushoto), akikabidhi boti za Uulinzi na Uusalama baharini, kwa vijiji vya Mkinga na Tanga Jiji. Boti hizo zimetolewa na Shirika la Mwambao Coastal Community Network Tanzania, Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi
Picha: Boniface Gideon
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Matilda Buriani (watatu kushoto), akikabidhi boti za Uulinzi na Uusalama baharini, kwa vijiji vya Mkinga na Tanga Jiji. Boti hizo zimetolewa na Shirika la Mwambao Coastal Community Network Tanzania, Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi

HALMASHAURI za Wilaya ya Tanga, Muheza na Mkinga, zimepatiwa boti za ulinzi na usalama baharini, kwa ajili ya kuongeza nguvu za doria dhidi ya wahalifu na wavuvi haramu.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Matilda Buriani, akikabidhi boti hizo, Januari 27, 2027 katika Kata ya Chongoleani, alisema zinakwenda kuongeza nguvu kazi kwenye ulinzi na usalama baharini,

Alisema wahalifu hao, wamekuwa wakitumia fursa ya udhaifu wa kiulinzi kufanya matukio yanayoharibu mazingira ya bahari.

Boti hizo zimetolewa na Shirika la Mwambao Coastal Community Network Tanzania, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo 'WILD AID' kwa 'CMA' ya Kimtommwage, Kata ya Kigombe wilayani Muheza.

"Tunawashukuru sana Mwambao Coastal Community Network Tanzania, kwa msaada wenu, niwahakikishie kuwa, boti hizi zitakwenda kufanya kazi iliyokusudiwa na matokeo yake mtayaona.

Ni lazima kila mmoja wetu awe mlinzi wa Rasilimali za Bahari,ili tunusuru hali ya upatikanaji wa samaki na viumbe wengine kwa faida yetu sisi na vizazi vijavyo," alisisitiza Batilda

Batilda aliwataka wakazi wa vijiji vinavyouzunguka bahari kuacha tabia ya kujihusisha na uchafuzi wa mazingira na uvuvi haramu,

"Niwaombe wakazi mnaoishi pembezoni mwa bahari, kumbukeni maisha yenu kwa kiwango kikubwa yanategemea bahari, hivyo ulinzi na usalama baharini ni jukumu letu sote," aliongeza Batilda. 

Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi ya Shirika la Mwambao Coastal Community Network Tanzania, Hassan Kalombo, alisema boti hizo zimetolewa kwenye kijiji hicho kutokana na idadi kubwa ya wavuvi,

"Kijiji hiki ni moja ya vijiji ambavyo vina wavuvi wengi sana katika mkoa wetu na wakazi wake asilimia kubwa maisha yao yanaendeshwa kwa uvuvi, kwa hiyo sehemu ambayo ina watu wengi hata uhalifu nao unakuwa mwingi, tumeona tusaidie kuongeza nguvu za kiulinzi majini," aliongeza Kalombo. 

Aidha aliwataka wakazi wa vijiji ambavyo vimezungukwa na bahari kujiepusha na uhalifu wa majini, ili kuongeza wigo wa uzalishaji wa samaki,

Mratibu wa Shirika la Mwambao Coastal Community, Network Tanzania, Mkoa wa Tanga, Ahmed Salim, alisema boti hizo ni mwendelezo wa kusaidia jamii iishiyo mwambao wa bahari na mapambano dhidi ya uhalifu wa majini hususani uvuvi haramu na uchafuzi wa mazingira,

"Moja kati ya majukumu yetu kama shirika, ni kusaidia jamii kwa kugusa maisha ya moja kwa moja, tumekuwa tukisaidia mitaji, elimu ya mazingira na kuwawezesha kupanda miti.

Boti hii tunaamini itasaidia kunusuru kizazi chetu na cha badae, hivyo niwaombe muitunze, ili tutokomeze wahalifu majini," aliongeza Ahmed.

Jacob Naila, Ofisa Mfawidhi Idara ya Uvuvi Kitengo cha Doria kutoka Wizara ya Uvuvi, alisema wanatarajia kufanya kazi ya doria usiku na mchana katika maeneo yote ya Bahari,

"Kupitia Boti hii, tunatarajia kufanya doria kwenye maeneo mbalimbali ya bahari, tunaomba mtupatie boti nyengine, ili tuongeze wigo ya doria katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Tanga," aliongeza Mbaga.