TTB yatangaza ‘vita’ na kampuni zinazowakopa wakulima

By Halima Ikunji , Nipashe
Published at 09:49 AM Apr 23 2024
Mkurugenzi wa TTB, Stanley Mhozya.
Picha: Maktaba
Mkurugenzi wa TTB, Stanley Mhozya.

BODI ya Tumbaku Tanzania (TTB) imesema itazichukulia hatua kampuni zenye madeni ya msimu uliopita, ikiwa ni pamoja na kutozipa leseni ya ununuzi kwa msimu wa mwaka 2024/25.

Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi wa TTB, Stanley Mhozya na kusema kuwa kampuni za ununuzi zinazodaiwa na wakulima wa tumbaku ama ushuru wa halmashauri wanapaswa kukamilisha madeni hayo ili kupata leseni hiyo.

Mkurugenzi huyo alisema uzalishaji wa tumbaku unaongezeka kila mwaka kutoka kilo milioni 37 kwa mwaka 2023 mpaka kufikia kilo 180 kwa msimu huu.

Alisema mvua ingekuwa ya wastani uzalishaji wa tumbaku nchini ungeweza kufikia kilo milioni 215 zimeshindwa kufikiwa kutokana na mvua kubwa kunyesha kwani wakulima walikuwa wakiweka mbolea inakwenda na maji.

Alisema kufafanua kwamba kutokana na hali ya mvua hiyo ilisababisha mabani mengi ya kukaushia tumbaku kuanguka na hivyo wakulima kukosa kitu cha kukaushia tumbaku yao.

Alisema kwamba tatizo lingine ni ukosefu wa kamba za kufungia tumbaku kuchelewa kuwafikia wakulima kwa wakati na kusababisha zao la tumbaku kukosa ubora hali hiyo ilijitokeza mwaka jana na kwa mwaka huu haitojirudia.

Alisema kampuni za ununuzi wa tumbaku nchini zimeongezeka kutoka tatu hadi kufikia 12 ambazo zilipewa leseni baada ya serikali kuanza kuboresha mazingira mazuri ya uboreshaji ya uwekezaji.