KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda amesisitiza dhamira ya TRA kuendelea kuhudumia walipakodi kwa kuagiza ofisi zote za TRA mikoa yote kutenga siku ya Alhamisi kuwa mahususi kusikiliza kero na kutatua changamato za walipakodi.
Alitoa agizo hilo jana jijini hapa wakati akizungumza na wafanyabiashara kwa nyakati tofauti katika ziara yake inayoendelea Kanda ya Ziwa.
"Ili kuongeza ufanisi, tumekubaliana kila Alhamisi kuwa siku maalumu kwa ajili ya kusikiliza walipakodi," alisema Kamishna Mkuu Mwenda na kuongeza kuwa haimaanishi kwamba siku nyingine hawatasikilizwa, bali Alhamisi itakuwa siku maalumu, hivyo walipakodi wasisite kwenda TRA kupata huduma.
Kamishna Mkuu wa TRA pia aliwahimiza walipakodi kupakua na kuitumia app ya TRA SIKIKA ambayo aliizindua hivi karibuni, kutoa maoni, kero, ushauri na mependekezo ambayo yatamfikia moja kwa moja na atayafanyia kazi.
Baadhi ya wafanyabiashara walimpongeza na kumshukuru Kamishna Mkuu kwa kuwasikiliza na kujenga ukaribu na walipakodi, jambo ambalo wanaamini litachochea ulipaji kodi kwa hiari nchini.
Kamishna Mkuu Mwenda anaendelea na ziara kwa kutembelea, kusikiliza, kuzungumza na kutatua kero zinazowakabili walipakodi ili kujenga ukaribu na kuboresha uhusiano kati ya TRA na walipakodi na hivyo kuongeza ulipaji kodi wa hiari.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED