MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imetakiwa kutoa elimu ya aina ya kodi wanazopaswa kutoa wawekezaji kabla ya kuanza kufanya biashara ili kuepuka malumbano baina yao na maafisa wake.
Rai hiyo imetolewa na Mwakilishi wa Wazalishaji wa Mvinyo wa Kampuni ya CETAWICO ya jijini Dodoma, Catherine Mwembe wakati akitoa maoni kuhusu kuboreshwa kwa mfumo wa ulipaji Kodi nchini.
Maoni hayo alitoa juzi katika kikao baina ya walipakodi na Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi nchini inayoongozwa na Balozi Ombeni Sefue.
Catherine, alisema wawekezaji nchini wanatakiwa kuelimishwa aina ya kodi wanapaswa kulipa kwenye biashara zao nchini ili kuepusha malumbano hayo, baadhi kufunga biashara na kuwakimbia maafisa hao.
Alilalamikia utitiri wa kodi kwa madai umekuwa kero kwa walipakodi na chanzo cha wengi wao kukwepa kulipa kwa kufunga biashara na kuwakimbia maofisa hao wanapofika kwenye biashara zao.
"Tunaomba serikali itoe elimu kwa wawekezaji, wafanyabiashara na wananchi kuhusu aina za kodi wanazopaswa kulipa kusaidia kupunguza kero na mvutano na maofisa wa TRA wakati wa kudai kodi," alisema.
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Mafuta wa Kanda ya Kati, Faustine Mwakalinga, alisema serikali inapaswa kutengeneza mfumo wa kukusanya kodi eneo moja ili kupunguza gharama na kupanua wigo mapato.
Mwakalinga, alisema suala si kodi nyingi bali changamoto iliyopo maofisa 15 wa mamlaka hiyo wanatumwa kwa mfanyabiashara mmoja kukusanya kodi kila moja kwa wakati wake na kusababisha usumbufu.
"Tunaomba serikali iliangalie suala hilo kwa karibu zaidi ili kuondoa usumbufu wakati wa kudai kodi kwa walipa kodi," alisema.
Kwa upande mwingine, Mwakalinga aliishauri TRA kuimarisha kitengo cha ukusanyaji kodi ili kuwarahishia walipa kodi kulipa kodi stahiki kwa wakati.
Tume hiyo iko mkoani Dodoma kupokea maoni kutoka kwa walipa kodi ili kurejea na mapendekezo ya nini kifanyike kuboresha mfumo wa ulipaji kodi nchini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED