TCRA yajipanga kudhibiti uhalifu fedha mtandaoni

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:43 AM Jun 17 2024
Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Maharage Chande.
Picha: Mpigapicha Wetu
Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Maharage Chande.

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema inaendelea kuweka jitihada za kupambana na kudhibiti uhalifu mitandaoni, ikiwamo huduma za kifedha kutokana na kuongezeka mifumo mipya ya mawasiliano ya teknolojia.

Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki jijini Arusha na Meneja wa Huduma za Posta wa TCRA, Cecilia Mkoba, wakati akizungumza katika jukwaa la wakurugenzi wakuu 42 wa Posta na taasisi za udhibiti mawasiliano waliokutana kuweka mipango ya maendeleo ya Sekta ya Posta Barani Afrika (PAPU).

“Nchi yetu tuna bahati kwamba hatujapata uhalifu kwenye sekta ya fedha na tunachoangalia ni kwamba tutaendeleza uelewa wa wananchi kwa sababu TCRA ni mwezeshaji katika mitandao, ili kudhibiti vitendo hivyo na kuvizuia,” alisema.

Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Maharage Chande, alisema kadiri maendeleo ya teknolojia yanavyozidi kukua na shughuli za posta zilizokuwa zinafanyika awali zinapungua na hivyo wanakutana kuweka mikakati ya jinsi Bara la Afrika linavyoweza kutumia teknolojia kuboresha huduma za posta ikiwamo duka mtandao, usafirishaji na kuongeza ubunifu.

“Wiki hii tumeanza mikutano, mmoja ni huu wa mazungumzo ya kiposta ambao kikubwa tutamzungumzia teknolojia na jinsi itakavyoboresha huduma za posta. Pia tutaangalia jinsi kanuni zitasaidia sekta ya posta kukua zaidi,” alisema.

Chande alisema kuwa katika eneo la teknolojia, Tanzania imepiga hatua; Shirika la Posta limeanza kutoa mafunzo ya usimikaji mifumo ya kiposta kwa mataifa mengine ambako wataalamu kutoka Tanzania wanatumika katika nchi mbalimbali barani la Afrika kubadilishana uzoefu kwenye shughuli hizo.

“Mfano leo tumepokea wataalamu wetu waliokwenda kufundisha na kusimika mifumo Zimbabwe. Tanzania kwenye mtandao tuko mbele. Hivi sasa katika mafunzo na usimikaji mifumo ya  kiposta, wataalamu wetu wanatumika katika Bara la Afrika kufanya shughuli hizi,” alitamba.

Akizungumzia changamoto za sekta ya posta na usafirishaji barani Afrika, Mjumbe wa Bodi ya Tume ya Mawasiliano Uganda, Paul Odoi, alitaja changamoto hizo ni pamoja na ongezeko la matumizi ya teknolojia, akisisitiza kuwa matumizi ya teknolojia yakizingatiwa yatasaidia kukuza sekta hiyo.

Kikao hicho ni mwendelezo wa Mkutano wa 42 wa Baraza la Utawala la Umoja wa Posta Afrika (PAPU), uliofanyika kwenye makao makuu ya umoja huo.