Kunenge: Fedha ndio zitatatua kero za wananchi sio asilimia za kwenye makaratasi

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 08:51 AM Jun 26 2024
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge.
Picha: Julieth Mkireri
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kinachokwenda kutatua kero za wananchi ni fedha na sio asilimia zinazoandikwa kwenye makaratasi.

Amesema kila halmashauri sasa inatakiwa kujikita kwenye matumizi yenye tija kwa kuibua vyanzo vipya vya mapato vitakavyoongeza mapato kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

Kunenge ameyasema hayo aliposhiriki katika kikao cha Baraza Maalumu la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG).

Amesema mkoa huo kwasasa umelenga kutengeneza, kukusanya na kuwa na matumizi yenye tija kwa kuonyesha hali halisi ya kinachoandikwa kwenye karatasi na maisha ya wananchi.

"Asilimia haikupi uwezo wasaidie kutoa huduma kwa wananchi, kinachoenda kutatua kero ni fedha sio asilimia, mkoa wetu sasa tunajikita kwenye matumizi yenye tija kwa kutoa matokeo mazuri ya mabadiliko ya maisha ya wananchi," amesema.

Akizungumzia kuhusiana na uzalishaji wa hoja Kungenge amesema hoja za ukaguzi sio za Mkurugenzi ni za Mkuu wa idara hivyo katika awamu ijayo kila mmoja anatakiwa akiwasilisha alizozalisha na kuelezea sababu zake kwamba kwa kufanya hivyo hakuna hoja zinazozuilika zitakazozalishwa.

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Pwani, Rashid Mchatta amepongeza utendaji kazi wa Mkurugenzi  wa Halmashauri ya Kibaha Regina Bieda huku akiwataka watumishi kumpa ushirikiano kufikia malengo.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Makala almesema wanachohitaji kwao ni kuona hoja zilizo ndani ya uwezo wa Halmashauri zinafungwa na kuacha zilizoshindikana kishughulikiwa na Mamlaka husika.

Awali Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Regina Bieda alisema Halmashauri hiyo kwa mwaka 2022/2023 hoja zilikuwa 49 kati ya hizo 23 zimefingwa na zilizobaki zinaendelea kufanyiwa kazi  hususani kwa zile zilizopo ndani ya uwezo wao.

Bieda pia ameahidi kuzingatia ushauri na maelekezo wanayopewa na kuepuka kuzalisha hoja mpya katika Halmashauri hiyo.