TARI yaanzisha kampeni upandaji miti ya matunda

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:01 AM May 09 2024
Kitalu cha miti.
Picha: Maktaba
Kitalu cha miti.

KITUO cha Utafiti wa Kilimo cha TARI Mlingano wilayani hapa Mkoa wa Tanga kimeanzisha kampeni ya kuhamasisha upandaji miti ya matunda na mazao ya viungo ili kuimarisha lishe bora nchini na kukabiliana na utapiamlo kwa watoto.

Jana, Mkurugenzi wa Kituo hicho, Catheline Senkoro alisema kuwa kutokana na tatizo la lishe kuwa tishio nchini, TARI imeanza kuwahimiza wananchi kupanda miti hiyo na mazao ya viungo katika mikoa tisa ya Tanzania Bara. 

 Senkoro, alisema hadi sasa wana miche 16,153 ya miti ya kivuli, mbao, limao, embe, michungwa, migomba, kokoa na mipapai.

 "Hiyo miche ya viungo ni mdalasini, karafuu na tangawizi,"alisema Senkoro.

 Wakati huo huo; Mbunge wa Muheza na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma ametoa msaada wa majiko ya gesi 135 kwa mama lishe katika vijiji vya Lusanga na Tanganyika.

Akizungumza kabla ya kugawa majiko hayo, Mbunge huyo, alisema ni kwa ajili ya kuwasaidia kuepuka gharama kubwa ya nishati ya mkaa na kuni.