ZAIDI ya ekari 1,000 za mazao katika Kijiji cha Makiba Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha zimekauka kwa ukame kutokana na kukosa maji kwa ajili ya umwagiliaji ya mfereji wa Makiba.
Kwa miaka kadhaa, mfereji huo umekuwa tegemeo kwa wakulima zaidi ya 5,000 wa kijiji hicho na vya jirani wa mazao hayo ya mahindi, maharage, migomba, mihogo na mboga.
Kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya wakulima, akiwamo Athanas Sumari, alisema hali ya maisha yao kwa sasa ni mbaya baada ya mazao yao kukauka.
Sumari, alisema baadhi ya watu wenye nguvu kuliko wao, wamefunga maji hayo ya mfereji na kuyatumia kwenye mashamba yao makubwa na kusababisha mazao yao kukauka.
“Hali ni ngumu kweli kweli kwa upande wetu wakulima kwa kuwa mazao yetu yamekauka na hatua zisipochukuliwa athari itakuwa kubwa na tutaathirika kabisa,” alilalamika.
Mkulima mwingine, Joseph Justo, alisema wamepanga kuandamana kwenda kwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru kufikisha kilio chao cha kukatiwa maji.
Justo, alisema baadhi ya wakulima wakubwa kwenye mashamba yaliyoko Doli, wamefunga mfereji huo unaotiririsha maji kwenda kwenye mashamba yao na kuathiri mazao yao kwa kukauka.
Pius Mmassy, alisema baadhi yao wamechukua mikopo benki na taasisi za fedha na kwamba anaona dalili ya kushindwa kurejesha mkopo kwa kuwa mazao yake yamekauka kwa ukame.
“Tunaomba serikali iingilie kati suala hili kwa kuwa wakulima tutakuwa masikini kutokana na mikopo tuliyoichukua tutashindwa kuilipa nani kutaifishwa mali zetu,” alisema.
Katibu wa mfereji huo katika eneo la Makiba, Elieza Kisaka, alisema kuna mtumishi wa idara ya umwagilia wa wilaya hiyo (hakumtaja jina), alitoa maelekezo ya maji kufungwa katika mfereji huo.
Kisaka, alisema mtumishi huyo, amesababisha maji yanayotiririka kutoka mfereji wa Doli hadi Kijiji cha Makiba kukatwa na kuzua taharuki hiyo kwa wakulima hao kwa mazao ya kukauka.
Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Makiba, Godlisten Lema, aliwapongeza wakulima hao kudai haki zao kistaharabu kwa kufuata hatua bila kufanya uharibifu wowote.
“Suala hili nimelifikisha kwenye Ofisi ya Ofisa Tarafa ya Mbuguni kwa ajili ya kufuatilia na kuchukulia hatua zaidi kwa waliosababisha maji kufungwa,” alisema Lema.
Diwani wa Kata ya Makiba, Samson Laizer, alisema ili kuhakikisha changamoto hiyo inapatiwa ufumbuzi inatakiwa mapendekezo manne yaliyotolewa yafanyiwe kazi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED