Serikali yasuka mpango mageuzi sekta ya mifugo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:04 AM Jun 17 2024
Maonesho na mnada wa mifugo.

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amesema serikali imeandaa mpango wa mageuzi ya sekta ya mifugo utakaosaidia kupata ufumbuzi wa changamoto zinazokabili sekta hiyo nchini.

Dk. Biteko aliyasema hayo jana wilayani Kibaha, Pwani wakati akifunga maonesho na mnada wa mifugo kwa mwaka 2024. 

“Wizara msichoke wala msiache kuwapa elimu wafugaji wetu, lazima tukubali  kuwa wamekuwa hivyo kwa miaka mingi, mabadiliko lazima yatokee na lazima tujue  kuwa maeneo mengi yanayohitaji ardhi yanaongezeka, ikiwa ni pamoja na mifugo lakini ardhi haiongezeki. 

“Hivyo, tuendelee kuwapa elimu ya ufugaji kisasa  na kuhimiza wafugaji waje kwenye maonesho kama haya ili wapate ujuzi na teknolojia itakayowasaidia,” aliagiza Dk. Biteko. 

Dk. Biteko aliwataka wafugaji wasijione dhaifu wala wanyonge, akitolea mfano kuwa unaweza kukuta mfugaji ana ng’ombe 1,000, huwezi kumuita maskini kwa kuwa ng’ombe hao wanaweza kuwa mtaji; kinachohitajika ni namna anavyoweza kubadilisha maisha yake kwa kutumia hao ng’ombe alionao. 

Naibu Waziri Mkuu huyo alisema kuwa ni vyema maonesho hayo ya mifugo yakafanyika kikanda ili kuwafikia wakulima wengi zaidi nchini, ikiwa ni pamoja na kuwasaidia kupata ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili kama vile mbegu bora za mifugo au kujua teknolojia za kisasa za ufugaji. 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti, alipongeza washiriki na wadhamini wa maonesho hayo ya mifugo ambayo yanalenga kutoa elimu kwa wafugaji ili kuleta tija. 

“Maonesho haya ni ya muhimu na kwa mwaka huu tumeyawekea nguvu zaidi kwa kuwa yanaleta matokeo  makubwa na kwa kuwa yamekuwa maelekezo ya viongozi wetu wa serikali kuwa wafugaji wetu wasifuge kizamani.  

“Lazima sasa ifike mahali wafugaji wetu waondokane na ufugaji wa kizamani kwa mwamvuli wa kimila, na sisi wizara tumekuwa tukitoa elimu mara nyingi kupitia wataalamu wetu  na maofisa ugani licha ya wafugaji hawa kuwa na mwamko mdogo wa kufuga kisasa,” alisema Mnyeti.  

Alitolea mfano kuwa wafugaji hutembea umbali mrefu kutafuta malisho na matokeo yake mifugo inafika ikiwa imechoka na kuwa serikali imeendelea kutenga maeneo ya malisho ili kusaidia wafugaji nchini. 

“Tunatoa elimu ya kufuga kisasa kwa kunenepesha mifugo na kuuza hata ng’ombe mmoja kwa Sh. 500,000 au zaidi badala ya Sh. 200,000. Wafugaji lazima wajue ng’ombe ambaye hajafugwa kisasa, hajapata chanjo au akiugua anapewa tu dawa kiholela, hawezi kuuzwa nje ya nchi kwa sababu hana ubora,” alisema Mnyeti.