Serikali yagawa hekari 5,113 za Msitu wa Hifadhi ya Kuni

By Christina Haule , Nipashe
Published at 06:16 AM Apr 19 2024
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Judith Nguli.
Picha: Maktaba
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Judith Nguli.

SERIKALI wilayani Mvomero mkoani Morogoro imezindua ugawaji wa hekari 5,113 zilizoachiwa na serikali kwa wananchi katika Msitu wa Hifadhi ya Kuni eneo la Makunganya.

Eneo hilo awali liliwekwa zuio kwa muda wa mwaka mmoja kutoendelezwa baada ya kuvamiwa maeneo bila kufuatwa taratibu.

Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Judith Nguli aliyasema hayo wakati wa kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na wananchi wa eneo hilo.

Judith alisema kufuatia maelekezo ya Serikali kupitia kamati ya mawaziri nane wa kisekta waliopita kwenye eneo hilo wakati wa mgogoro huo Serikali imeamua kutoa viwanja hivyo kati ya eneo lililokuwa zaidi ya hekari 30,000 za msitu wa hifadhi unaomilikiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Nguli alisema upimaji wa viwanja hivyo umefanywa tangu mwaka jana ambapo tayari viwanja 14,000 vimeshapimwa na zoezi linaendelea kwa ajili ya kukamilisha viwanja 19,000 ambavyo vinapaswa kutolewa kwa wananchi.

Alisema zoezi la ugawaji viwanja hivyo litaanza baada ya wiki mbili kutoka kikao hicho ambapo wananchi watatakiwa kulipia ndani ya miezi sita kulingana na gharama zilizopangwa.

Aidha, aliwataka wananchi hao kuona umuhimu wa kulipa malipo ya viwanja hivyo kwa wakati bila kuwa na maombi mengine.

Pia, aliwaomba wananchi hao kulipa gharama kwenda sambamba na muda sababu wasipolipa kwenye muda watachukua hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo ikiwemo kiwanja kugawiwa kwa mtu mwingine.

Hata hivyo, aliwahakikishia wananchi hao kutoona shida kulipa gharama za viwanja hivyo sababu eneo hilo tayari limeshapewa hadhi ya kuwa mji maarufu kwa kupewa jina la Suluhu New City.

Alisema eneo hilo linatarajiwa kuwekwa miundombinu yote muhimu ikiwemo shule, hospitali, soko, barabara na madaraja katika sehemu korofi na hivyo kupata wawekezaji na kukua kiuchumi kwa namna moja au nyingine.

Mtaalamu wa mipango na mambo ya ardhi kutoka Wizara ya Ardhi, Julius Mwakafwila alisema viwanja hivyo vimegawiwa katika kanda tatu.

Alisema kanda ya kwanza ni kuanzia Barabara Kuu ya Morogoro -Dodoma hadi kulipokuwa kunafanyika mkutano awali ambako kutalipiwa mita moja ya mraba kwa Sh. 3000.

Mwakafilwa alisema kanda ya pili itakuwa kutoka walipokuwa wakifanyia mkutano awali hadi kwenye ghorofa ambao watalipa mita moja ya mraba Sh. 2000 na kutoka pale hadi mwisho watalipa kila mita moja ya mraba Sh. 1000.

Alisema kwa wale wenye nyumba na mapagala watalipwa Sh.2000 kwa mita moja ya mraba kuanzia wale wa barabarani hadi kwenye ghorofa, huku wale wa kutoka kwenye ghorofa hadi mwisho wakilipia Sh. 1000.

Baadhi ya wananchi wa maeneo hayo akiwemo Baraka Casbert alimuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuwaongezea muda wa malipo na kupunguza gharama ya malipo kutoka Sh.2000 kwa mita moja ya mraba na kuwa Sh. 1000 hasa wale wenye nyumba kutokana na kuwa na kipato kidogo.

 Moses Mtinde alisema awali walikumbwa na adha mbalimbali ikiwemo za kubomolewa nyumba, kwamba walishindwa hata kuzirekebisha baada ya kuwekewa zuio.