Pensheni za wazee sasa kupitia benki

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:27 AM Apr 04 2024
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dk. Sada Mkuya Salum.
MAKTABA
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dk. Sada Mkuya Salum.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dk. Sada Mkuya Salum, amesema wazee wote wanaolipwa fedha za pensheni jamii watafunguliwa akaunti ili malipo yapitie benki na kuepusha matukio ya udanganyifu na vitendo vya utapeli.

Waziri Mkuya alisema hayo jana, alipofanya mazungumzo na wazee wanaopokea fedha za pensheni jamii katika ukumbi wa Sheikh Idris Abdulwakil, Kikwajuni, Mjini Unguja na kuwakutanisha viongozi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.

Alisema kwa muda mrefu serikali imekuwa  ikifanya malipo ya pensheni jamii kwa wazee waliofikisha umri wa miaka 70 katika utaratibu ambao si rasmi wa kulipa mikononi kupitia katika vituo walivyokubaliana na wazee.

Dk. Mkuya alisema utaratibu huo kwa kiasi kikubwa umekuwa na changamoto nyingi ambazo kwa nyakati tofauti zimeibua malalamiko ikiwamo baadhi ya wazee kushindwa kufikiwa na kupata fedha hizo.

Alisema kwa sasa serikali imeamua wazee wote wanaostahili kulipwa pensheni jamii, kufungua akaunti kupitia Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) kwa ajili ya kupata malipo halali.

“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tumeanza mfumo wa malipo ya fedha za pensheni jamii kwa wazee kwa njia ya benki hatua ambayo ni salama  yenye uhakika wa fedha za wazee kuwafikia moja kwa moja,” alisema.

Aidha, alisema mfumo wa malipo ya pensheni jamii kwa wazee wastaafu kupitia benki utaondosha udanganyifu ambao uliwahi kufanywa na watendaji wa wizara ambao si waaminifu.

Naye Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Rikizi Pembe Juma, alisema uamuzi wa kuwafunguliya akaunti wazee wanaolipwa fedha kupitia pensheni jamii ni sahihi na wenye lengo la kuondoa usumbufu kati ya watendaji wa wizara pamoja na wazee kwa ujumla.

Alisema uamuzi wa kuwalipa wazee pensheni jamii unatokana na serikali kutambua mchango mkubwa wa wazee ambao walifanya kazi kubwa ikiwamo katika kuleta uhuru pamoja na kutunza familia ambazo matokeo yake ndiyo jamii iliopo sasa.

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrisa Kitwana Mustafa, alizipongeza wizara  hizo kwa kazi kubwa zinayofanya katika kutekeleza na kusimamia jukumu la kulipa pensheni jamii ya wazee waliofikisha umri wa miaka 70.

Alisema wazee wanatakiwa kuenziwa, hivyo kitendo cha wizara mbili kuweka mazingira mazuri ya kulipwa pensheni jamii kinastahili kuungwa mkono.

Zaidi ya wazee 25,000 wanalipwa pensheni jamii na serikali ya Zanzibar na miongoni mwa vigezo muhimu ni kufikia umri wa miaka 70 ambayo kwa sasa imeongeza na kufikia kiwango cha Sh. 50,000 kwa mwezi.