Manufaa kongamano ufuatiliaji tathmini yabainishwa

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 10:59 AM Sep 17 2024
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dk. Jim Yonazi.
Picha: Mpigapicha Wetu.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dk. Jim Yonazi.

KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dk. Jim Yonazi, amesema kongamano la ufuatiliaji na tathmini litatoa fursa kwa wadau wote, ikiwamo serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na sekta binafsi kushirikiana katika kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji ambayo itachochea maendeleo nchini.

Aidha, alitoa wito kwa wadau katika sekta hiyo na Watanzania kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika kongamano hilo la tatu la wiki ya ufuatiliaji, tathimini na kujifunza linalotarajiwa kufanyika kuanzia leo hadi Septemba 20, mwaka huu, visiwani Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na kiongozi huyo, kongamano hilo la kitaifa nchini limekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha eneo hilo serikalini kwa kuongeza uwezo wa wataalamu wa ufuatiliaji na tathimini.

“Kupitia warsha hiyo, mafunzo, na midahalo, washiriki hujifunza mbinu mpya, zana na teknolojia za kisasa za ufuatiliaji na tathmini ambazo zinaweza kutumika kuboresha utendaji wa miradi ya maendeleo," alisema Dk. Yonazi.

Kongamano hilo pia linalenga kukuza uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa sera na miradi ya maendeleo, kwa kuleta pamoja wadau mbalimbali wakiwamo watendaji wa serikali, wabunge, mashirika yasiyo ya kiserikali na wananchi.

Alisema kongamano hilo linatoa fursa ya kujadili jinsi ufuatiliaji na tathmini inaweza kutumika kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa ufanisi na uwajibikaji.

Umuhimu wa ufuatiliaji na tathmini katika maendeleo ya nchi na inachangia kwa namna mbalimbali kuboresha utendaji wa serikali na sekta binafsi.

“Ufuatiliaji na tathmini husaidia kubaini jinsi rasilimali zinavyotumika na kuhakikisha kwamba fedha na muda zinalenga malengo yaliyokusudiwa hii inasaidia kuongeza uwazi katika utekelezaji wa miradi na programu za maendeleo.

"Kwa kutumia data sahihi, watunga sera wanaweza kuchambua jinsi programu za maendeleo zinavyotekelezwa na matokeo yanayopatikana, hii husaidia kufanya maamuzi ya sera yaliyo sahihi zaidi kwa kuzingatia ushahidi wa kiutendaji,” alisema Dk. Yonazi.

Hata hivyo, alisema matokeo ya ufuatiliaji na tathmini yanawezesha serikali na wadau wa maendeleo kupima mafanikio na changamoto za miradi mbalimbali ya maendeleo, pia yanatumika kurekebisha au kuboresha programu zinazoendelea kutekelezwa.

Vile vile, alitoa wito kwa wadau mbalimbali kushiriki ili kuongeza uelewa wa masuala ya ufuatiliaji na tathmini, kupata maarifa ya ubunifu pamoja na kushirikishana uzoefu katika eneo hilo nchini.

Mwisho