Jafo: Bila elimu hatuwezi kufikia uchumi wa viwanda

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 09:55 AM Apr 23 2024
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Selemani Jafo.
Picha: Maktaba
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Selemani Jafo.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Selemani Jafo amesema Tanzania haiwezi kufikia lengo la kuwa nchi ya uchumi wa viwanda kama haitawekeza kweye elimu.

Alibainisha hayo jana jijini hapa, alipokuwa akizungumza na wazazi na wanafunzi kwenye mahafali ya kwanza ya kidato cha sita na uzinduzi wa maabara ya kisasa ya masomo ya sayansi katika Shule ya Sekondari ya Fountaine Gate ya jijini Dodoma.

 Alisema ili kufikia azma ya uchumi ya viwanda kama taifa linapaswa kuwekeza katika sekta ya elimu ili kupata rasilimali watu ya kutosha, ili kuwatumia katika viwanda vitakavyo anzishwa nchini.

“Hatuwezi kufikia azma ya kuwa na taifa la uchumi wa viwanda kama hatutawekeza kwenye elimu, ndiyo maana serikali imeweka jitihada katika uwekezaji kwenye sekta ya elimu kujenga madarasa, nyumba za walimu na kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji katika sekta ya elimu” alisema.

Aidha, aliipongeza shule hiyo kwa kuanza kutoa masomo kwa kutumia tahasusi mpya ambazo zinajikita katika masuala ya uhifadhi wa kimazingira ili kukabiliana na atahri za mabadiliko tabianchi.

Jafo alisema hali hiyo itasaidia Watanzania kuwa na uelewa mpana wa athari zitokanazo na mabadiliko tabianchi na kukabiliana nazo kwa kutunza mazingira. 

Mkuu wa Shule ya Fountaine Gate Dodoma, Spicious France alisema shule hiyo inawalea wanafunzi kufuata misingi mitatu ambayo ni maarifa, hekima na vipaji.

Alisema: “Mheshimiwa katika eneo la maarifa shule imefanikiwa kufanya vizuri kwenye mitihani ya ngazi mkoa kwa kushikia nafasi ya tatu kiwilaya na nafasi ya tano kimkoa katika mitihani ya utimilifu kwa mwaka wa masomo 2023/2024, malengo yetu ni kuhakikisha kila mwafunzi wa kidato sita anapata daraja kwa kwanza katika mtihani wa taifa utakao anaza Mei 6, mwaka huu”.