Dawa kuwaangamiza ‘Kantangaze’ yagundulika

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 10:04 AM Jan 04 2025
Dawa kuwaangamiza ‘Kantangaze’ yagundulika.
Picha: Mtandao
Dawa kuwaangamiza ‘Kantangaze’ yagundulika.

WAKULIMA wa nyanya Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, wanaopoteza jasho lao shambani kutokana na kusumbuliwa na wadudu waharibifu wa mazao ‘Kantangaze’ (Tuta Absulute), sasa wamepata ahueni baada ya watafiti kugundua namna mpya ya kuwaangamiza kwa kutumia homoni maalum.

Mtaalamu wa Kilimo Biashara wa Shirika la World Vegetable Center, Judith Assenga, akizungumza jana na wakulima wa nyanya katika shamba mafunzo Kijiji cha Masaera, Kata ya Makuyuni, alisema mdudu huyo amekuwa tishio kwa zao hilo kutokana na uwezo wake wa kushambulia na kuhatarisha uhakika wa mavuno kwa asilimia 80 mpaka 100.

Mradi huo wa Agroveg, unaotekelezwa na Shirika la World Vegetable Center katika Wilaya ya Moshi, umeanza kuleta tija kwa kupunguza uzalishaji wa nyanya kwa kutumia viuatilifu vya sumu. Mradi huo wa miaka mitatu, unafadhiliwa na Biovision kupitia Taasisi ya ICIPE.

“Kwenye zao la nyanya, tunajitahidi sana kupunguza matumizi ya dawa. Tunayo teknolojia ya kwanza, ambayo tunaita homoni maalum, ambazo zinavuta wale wadudu wa kantangaze.

“Tunatumia kilimo cha mzunguko, ambacho ukilima nyanya, mwisho wa siku ukivuna zile nyanya, hupaswi kurudia tena kulima nyanya na hiyo ndio mwarobaini wa kumwangamiza kantangaze.

“Nawashauri wakulima wajitahidi sana kuchukua hii teknolojia ya kuvuta na kusukuma wadudu (Push Pull Technology), kwa kutumia mazao mchanganyiko, kwa kuwa hii teknolojia ni nzuri kwao, kwa sababu inawapunguzia matumizi makubwa ya gharama shambani.

…Faida ya mkulima inapunguzwa sana na matumizi makubwa ya dawa shambani. Pili, nawashauri watuimie hii teknolojia kwa sababu ni teknolojia ambayo itamlinda yeye na afya ya mlaji.”

Mtaalamu wa Afya ya Mimea wa World Vegetable Center, Dk. Simon Boniface, alisema kuhusu afya ya udongo, kemikali zinaharibu sio tu afya ya viumbe vinavyokuwa juu ya ardhi, bali vile vinavyokuwa ndani ya ardhi.

Alisema kuna minyoo, ambao ni muhimu sana kwenye afya ya ardhi, lakini kuna vimelea kama fangasi na bakteria, ambao wanachakata yale masalia ya mimea ndani ya ardhi kuweza kutoa virutubisho ambavyo vinaweza vikatumika na mmea.

“Kwa mfano unaweka samadi kwenye shamba, vimelea ndivyo vinavyoichakata kwa kuivunjavunja ili yale madini ambayo mmea unaweza ukachukua. Lakini minyoo iliyopo inatengeza njia na mashimbo ambayo ni muhimu sana kwenye rutuba ya udongo, ambako kutakuwa na hewa na maji yakapita vizuri.

…Kama fangasi au bakteria, ambao wanawashambulia kantangaze, na wenyewe kwa pamoja tukichanganya kwa kutumia teknolojia tunayoita kitaalam Integrated Pastes Management (IPM), kwa Kiswahili tunawezasema kwa kutumia njia shirikishi na jumuishi kwa pamoja. Njia tofauti tunazichanganya kwa pamoja ili kupambana na tatizo lililopo.”