Asilimia sita ya wakazi H/shauri Njombe wanakula mayai

By Elizabeth John , Nipashe
Published at 09:13 AM May 09 2024
news
Picha: Mtandaoni
Mayai yaliochemshwa.

IMEELEZWA kuwa asilimia sita ya wakazi wa Halmashauri ya Mji Njombe mkoani Njombe ndiyo wanaokula mayai, huku unywaji wa maziwa ukiwa asilimia 16 jambo ambalo linafifisha jitihada za kupambana na udumavu.

Taarifa hiyo ni kwa mujibu wa Ofisa Lishe Halmashauri ya Mji Njombe, Michael Swai, aliyoitoa katika Kongamano la Wanawake la kuwajengea uwezo katika kutokomeza udumavu katika Tarafa ya Njombe Mjini.

Swai alisema wananchi wengi hawatumii mayai na maziwa ilihali ni miongoni mwa vyakula muhimu katika kupambana na udumavu, huku pia mimba za utotoni nazo zikitajwa chanzo cha kuongezeka udumavu na utapiamlo.
 
 “Lakini vile vile katika matumizi ya vyakula tuna asilimia sita tu ya wananchi ndiyo wanatumia mayai na asilimia 16  ndiyo wanatumia maziwa,” alisema Swai.

Naye Mratibu wa Huduma za Mama na Mtoto Halmashauri ya Mji Njombe, Grolia Mlowe alisema watoto wengi wanapata ujauzito bila ya kutarajia, hivyo wanajificha bila ya kutoa taarifa na kusababisha kutokupata huduma muhimu.

“Wanatakiwa kufika kwenye vituo vyetu vya afya ili kupata huduma kuhusu uzazi na namna ya kujizuia na ujauzito,” alisema Mlowe.

Awali Ofisa Tarafa wa Njombe Mjini, Lilian Nyemele, alisema kongamano hilo limekuja kwa lengo la kutokomeza udumavu, elimu ya ujasiriamali kwa wanawake pamoja na kueleza umuhimu wa matumizi ya bima.

“Kila mtaa wapate kinara wa lishe, kila ubalozi wa nyumba kumi utachagua kinamama wasiopungua watano ili kuwatambua wajawazito walioanza kliniki,” alisema Nyemele.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe, Kuruthumu Sadick, alisema ili kuweza kuleta tija inapaswa makongamano hayo yafanyike hadi katika maeneo ya vijijini.

Wakizungumza na Nipashe baada ya elimu hiyo mmoja wa wakazi wa mjini Njombe, Vumilia Bange, alisema waamini elimu hiyo inakwenda kuwakomboa watoto wao na kisha kuahidi kuanza kuzingatia malezi na mlo licha ya kuwa bize na majukumu na kutafuta maisha.