Ado amvaa Waziri Bashe, mpango uwezeshaji wakulima

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:07 PM Jul 26 2024
Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu.
Picha: Mpigapicha Wetu
Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu.

Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu amemueleza Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kuwa mipango ya uwezeshaji wa wakulima inapaswa kujikita vijijini ili kuwawezesha wakulima halisi na kuongeza tija katika uzalishaji.

"Kuna mradi huu wa BBT. Fikra ya kuwawezesha wakulima ni fikra njema. Lakini, mpango ulipaswa kujikita vijijini. Huko ndiko waliko Wakulima halisi. Mtindo wa wizara kukusanya vijana mijini, kuwapa mikopo, ardhi na nyenzo, hautaleta matokeo makubwa na mpango utafeli kama ilivyofeli mipango iliyotangulia ya kilimo" alisisitiza Ado

"Janga la ajira ni bomu linasubiri kuripuka. Ili kukabiliana nalo, pamoja na mambo mengine ni lazima tuboreshe kilimo na shughuli nyingine za uzalishaji vijijini kwa kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo za uhakika, bei nzuri za mazao na mikopo yenye riba nafuu kuongeza tija katika kilimo na ufugaji"-alisema Ado.

Katika hatua nyingine, Ado alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ibane matumizi na kuzuia ubadhirifu ili kuhakikisha kuwa inaajiri zaidi hasa kwenye maeneo ambayo yana mahitaji makubwa ya wafanyakazi kama vile walimu, madaktari na maafisa ugani.

"Serikali ya CCM imechoka kifikra. Kila Mwaka CAG anaonesha mabilioni ya Watanzania yanaliwa. Serikali ingeongeza udhibiti kwenye eneo hilo ingeweza kuokoa fedha nyingi na kuajiri wahitimu wengi zaidi ambao kwa miaka mingi bado wapo mtaani"- alisema Ado