Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga, imeunda timu ya mabalozi sita watakaosimamia usafi wa mazingira katika mitaa 35 ya manispaa hiyo.
Timu hiyo inaongozwa na Mzee Anderson Lymo (Mwenyekiti) na Alexander Kazimili (Katibu), wakishirikiana na Yona Bakungile, Pendo Bwakeo, Therezia Mahongo, na Arnald Bweichum.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita, alibainisha hatua hiyo leo 13/02/2025 wakati wa ziara yake ya kukagua hali ya usafi, ambapo aligundua mitaro kuziba na kusababisha maji ya mvua kuingia kwenye makazi ya wananchi.
Mabalozi hao watasimamia usafi, kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira, na kushirikiana na wadau wa mazingira. Wanaobainika kuchafua mazingira watachukuliwa hatua za kisheria. Aidha, Jeshi la Akiba litatatua tatizo la mitaro kuziba kwa kushirikiana na TARURA.
Mhita alisema kutakuwa na namba maalum itakayowekwa kwenye vipokea taka katika mitaa yote, ambapo wananchi wataweza kutoa taarifa za uchafuzi wa mazingira bila gharama yoyote.
Ofisa Mazingira wa Manispaa, Johannes Mwebesa, alikiri kuwepo kwa uchafuzi wa mitaro na kuwataka wananchi kufanya usafi ndani ya mita tano kutoka makazi yao. Alieleza kuwa kwa siku, Kahama huzalisha tani 171 za taka, huku asilimia 78.9 zikikusanywa.
Baadhi ya wakazi, kama Suzana Mussa wa Nyasubi, wamelalamikia magari ya kuzoa taka kutofika maeneo yao, hali inayowalazimu kulipa Sh. 1,000 kwa vijana kupeleka taka dampo, au kuzifukia ardhini, jambo linalohatarisha mlipuko wa magonjwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED