MABAO mawili yaliyofungwa na wachezaji wapya, Prince Dube na Clatous Chama, huku mengine yakipachikwa na Clement Mzize na Stephane Aziz Ki, yameifanya Yanga kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kupata ushindi wa magoli 4-0 dhidi ya wenyeji, Vital'O ya Burundi.
Kwa ushindi huo, mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga walikabidhiwa kitita cha Sh. milioni 20, kila goli likiwa na thamani ya Sh. milioni tano, ambazo zitakuwa zinatolewa katika kila mechi ya kimataifa na Rais, Samia Suluhu Hassan.
Dube alisajiliwa na Yanga akitokea Azam FC baada ya kuvunja mkataba wake huku Mzambia Chama kutoka kwa Simba alitua kama mchezaji huru kutokana na kumaliza mkataba wake na Wekundu wa Msimbazi.
Iliwachukua Yanga dakika tano kupachika bao la kwanza katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, ambapo kikanuni ilikuwa inacheza ugenini.
Bao hilo la Dube lilidumu mpaka timu hizo zilipokwenda mapumziko, lakini wenyeji Vital'O walikuwa wa kwanza kufika katika lango la Yanga kwa shambulio jepesi lililookolewa na nahodha, Bakari Mwamnyeto.
Alikuwa ni Nickson Kibabage aliyepelekewa pasi ndefu katika wingi ya kushoto, akabaki na kipa wa Vital'O, Hussein Ndayishimiye, lakini shuti lake la mguu wa kushoto lilitoka nje kidogo ya lango.
Dakika moja baadaye, Yanga ilifanya shambulizi lililofanana na hilo lililoipatia bao, Aziz Ki kwa mara nyingine aliuinua mpira mrefu wingi la kushoto uliomkuta, Dube eneo lile lile alilokuwepo Kibabage mwanzo, mwenzake hakufanya makosa, kwa mguu wa kushoto akaukwamisha wavuni dakika ya tano ya mchezo huo.
Baada ya bao hilo, Vital'O walionekana kuamka na kuamua kwenda mbele, lakini kwa mahesabu makali kwa sababu wanapopoteza mpira walikuwa wanarudi wengi langoni mwao.
Chama aliupata mpira akiwa katika eneo zuri, lakini shuti lake liliwababatiza mabeki wa timu pinzani dakika ya 18 na dakika ya 24 na 25, Vital'O walifanya mashambulizi langoni shuti la Fred Niyozideye lilipaa juu huku lile la Jean Nzeyimana, likiishia mikononi mwa kipa, Djigui Diarra.
Nusura Mwamnyeto aiandikie Yanga bao la pili dakika ya 35, aliporuka juu kuunganisha mpira wa kona uliopigwa na Aziz Ki, lakini uliondolewa kwenye mstari na beki Mrundi, Prince Musore.
Chama alipachika bao la pili dakika ya 68, baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Vital'O, baada ya shuti lililopigwa na Aziz Ki kugonga nguzo ya lango na kumfikia mfungaji aliyeukwamisha wavuni kirahisi.
Baada ya bao hilo, Chama alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Kennedy Musonda, mfungaji wa bao la kwanza, Dube naye akitoka na kuingia Mzize ambaye muda mchache baadaye akapachika bao la tatu.
Ilikuwa ni dakika ya 73, wakati mabeki wa Vital'O walipokuwa wakiuchezea mpira nyuma, mmoja akajaribu kumrudishia kipa, lakini kwa kasi, Mzize aliukimbilia na kumfanya kipa, Ndayishimiye aliyefanya kazi kubwa jana, kutokea, lakini alichelewa na hivyo kuifungia timu yake goli la tatu.
Aziz Ki, baada ya kosa kosa nyingi alifunga bao la penalti dakika ya 90 na kuifanya Yanga kuhitaji sare yoyote au kutofungwa idadi ya mabao zaidi ya manne katika mchezo wa marudiano utakaofanyika, Agosti 24, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Mshindi wa jumla wa mechi ya Yanga dhidi ya Vital'O, anatarajiwa kukutana na mshindi kati ya CBE ya Ethiopia au SC Villa ya Uganda.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED